Boma Hai FM

Wanachama HRT Saccos wahimizwa matumizi ya teknolojia

12 September 2026, 6:44 am

Pichani ni Wanachama wa HRT Saccos wakipatiwa elimu ya Matumizi ya teknolojia (Picha na Henry Keto)

Chama cha Akiba na Mikopo cha HRT Saccos kimeendelea kutoa elimu na mafunzo kwa wanachama wake kuhusu matumizi ya teknolojia kwa lengo lakutoa huduma kwa urahisi na usahihi pamoja na kuendana na kasi ya sayansi na teknolojia kwenye vyama vya ushirika.

Na Henry Keto, Hai-Kilimanjaro

‎Wanachama wa chama Cha Akiba na Mikopo Cha HAI RURAL TEACHERS SACCOS wameaswa kutumia teknolojia kwenye shughuli za chama kuongeza ufanisi  na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wanachama wa HRT SACCOS.

‎Wito huo umetolewa Septemba 11,2026 wakati wa Mkutano wa dondoo kwa Wanachama wa Tarafa za Lyamungo na Machame wenye lengo la Wanachama kujua maendeleo ya chama, pamoja na kutoa maoni yao kuelekea mkutano mkuu wa Chama unaotarajiwa kufanyika Novemba 7, 2026.

‎Afisa Tehama wa HRT SACCOS Emmanuel Bura ameeleza sababu za chama kutumia teknolojia, lengo ikiwa ni kurahisisha majukumu ya kazi kwa kupunguza Changamoto kwa Wanachama kufika ofisini ili kuhudumiwa kutokana na umbali kutoka majumbani Hadi ofisini na kupunguza msongamano kwa wanachama kusubiri huduma muda mrefu.

Sauti ya Afisa TEHAMA wa HRT SACCOS Emmanuel Bura
Pichani ni Mwenyekiti wa Chama cha HRT SACCOS mwalimu Alex Warioba (kushoto) na Afisa wa vyama vya ushirika wilaya ya Hai( Kulia)(Picha na Henry Keto)

Nae Meneja wa HRT SACCOS, Upendo Lyatuu amehimiza matumizi ya teknolojia kwa wanachama akiwataka kuendana na mifumo ya kisasa huku akieleza faida za mafunzo yaliyotolewa kwa wanachama kuhusu afya ya akili, bidhaa na huduma zinazotolewa na Chama kwa kuzingatia Masharti ya Chama, sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Vyama vya Ushirika Tanzania.

Sauti ya Meneja wa HRT SACCOS Upendo Lyatuu
Pichani ni Meneja wa Chama cha HRT SACCOS Upendo Lyatuu akitoa mada kuhusu bidhaa za chama (Picha na Henry Keto)

Nao wanachama walioshiriki Mkutano huo, wameshukuru uongozi wa chama kwa kuona umuhimu wa kuwaletea mafunzo ya afya ya akili kwa sababu ni tatizo kubwa kwasasa kwa wafanyakazi wengi, lakini pia kuwapa Elimu ya teknolojia katika kupata huduma, Pamoja na kupata taarifa za Chama. Wametoa wito kwa Wanachama wote kuendelea kushirikiana na kukitumia chama Cha HRT SACCOS kwani kina manufaa makubwa.

Baadhi ya Sauti za Wanachama wa HRT SACCOS waliohudhuria kikao hicho cha dondoo