Boma Hai FM

DC Bomboko awataka viongozi Hai kutoa elimu kampeni chanjo ya polio

26 August 2026, 3:57 pm

Pichani ni mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko (wa nne kulia)katibu tawala wilaya ya Hai Sospiter Magonera ( wa tatu kushoto)mganga mkuu wilaya ya Hai Dkt Itikija Msuya (wa pili kushoto) pamoja na viongozi mbalimbali katika kikao cha kampeni ya chanjo ya Polio( picha na Richard Salema)

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko, amesisitiza ushirikiano wa viongozi wa serikali, dini na jamii katika kuhamasisha wazazi na walezi kuwapeleka watoto walio chini ya miaka 10 kupata chanjo ya polio, huku zoezi hilo likitarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2026.

Na Gervas Mosha

Hai – Kilimanjaro

Mkuu wa Wilaya ya Hai Hassan Bomboko amewataka viongozi na watendaji katika ngazi za kata na vijiji kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kampeni ya chanjo ya polio, inayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 27 hadi 30, mwaka huu.

Bomboko amesema viongozi wanapaswa kutumia siku zilizobaki kabla ya kuanza kwa kampeni hiyo kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wazazi na walezi wenye watoto walio chini ya umri wa miaka 10, ili watoto hao wajitokeze na kupata chanjo.

Amesema chanjo hiyo ni haki ya kila mtoto mwenye umri chini ya miaka 10, hivyo ametoa wito kwa serikali, viongozi wa jamii, viongozi wa dini, wazazi, walezi, vyama vya siasa na taasisi binafsi kushirikiana katika kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai Dkt Itikija Msuya  amesema Halmashauri imejipanga kuhakikisha hakuna mtoto aliye chini ya umri wa miaka 10 anayekosa chanjo katika kampeni hiyo.

Sauti ya mganga mkuu wilaya ya Hai Itikija Msuya.

 Nae afisa afya wa wilaya ya Hai George Masawe, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha watoto wote walio katika kundi lengwa wanapata chanjo.

Sauti ya afisa afya wilaya ya Hai George Massawe.

Kampeni hiyo itafanyika kuanzia Agosti 27 hadi 30 mwaka huu, huku wananchi wakihimizwa kutoa ushirikiano kwa timu za afya zitakazohusika katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Pichani ni afisa afya wilaya ya Hai George Massawe akielezea jambo katika kikao cha kampeni ya chanjo ya Polio ya matone.( picha na Richard Salema)