Boma Hai FM
Boma Hai FM
2 August 2026, 9:23 am

Mradi wa From Aid to Trade (FA2T-2) unaotekelezwa na Shirika lisilo la Kiserikali la HAFEO umeanza kuleta matumaini mapya kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wilayani Hai , Kupitia mafunzo ya ufugaji wa kisasa, wafugaji wanajengewa uwezo wa kuongeza uzalishaji, kuboresha kipato na kujitegemea kiuchumi, huku kukiwa na mpango wa kuupanua mradi kutoka kata tatu hadi kata zote 17 za wilaya ya Hai.
Na Elizabeth Mafie
Hai – Kilimanjaro
Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kutumia elimu ya kisasa ya ufugaji ili kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuinua kipato cha kaya na kuchochea maendeleo ya uchumi wa jamii.
Wito huo umetolewa Agosti 1, 2026 na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Trael Mboya, alipomwakilisha Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe, katika mahafali ya wahitimu wa mafunzo ya mradi wa From Aid to Trade (FA2T-2) yaliyoandaliwa na Shirika la HAFEO yaliyofanyika katika kijiji cha Mungushi kata ya Masama Kusini wilaya ya Hai.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mboya amewataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kuwafundisha wafugaji wengine ili kuongeza tija katika sekta ya ufugaji wa maziwa na kuinua uchumi wa wananchi wa kata zote 17 za Wilaya ya Hai na kwamba vyeti walivyotunukiwa viwe chachu ya kuendeleza ufugaji wa kisasa na kuhakikisha matokeo ya mafunzo hayo yanaonekana kupitia ongezeko la uzalishaji wa maziwa.
Kwa upande wake, mfadhili wa mradi huo kutoka Shirika la HAFEO Dkt. Henk Kusters , amesema mradi huo ulianza mwaka 2023 ukiwa na lengo la kuwasaidia wafugaji kujitegemea kiuchumi kupitia ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa na kwamba mradi huo unalenga kuwajengea wafugaji maarifa na ujuzi utakaowezesha kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa lita tatu hadi nne za maziwa kwa ng’ombe mmoja kwa siku hadi kufikia wastani wa lita 15 kwa siku.

Dkt. Kusters amesema kwa sasa mradi unawahusisha wafugaji wapatao 400 wenye takribani ng’ombe 1,200 katika kata tatu za Wilaya ya Hai na endapo kila ng’ombe ataongeza uzalishaji kwa wastani wa lita 10 kwa siku, kutapatikana ongezeko la takribani lita 12,000 za maziwa kila siku, hatua itakayoongeza kipato cha wafugaji na kuimarisha uchumi wa eneo hilo.
Ameongeza kuwa matarajio ya HAFEO ni kupanua mradi huo hadi kufikia kata zote 17 za Wilaya ya Hai na kuendelea kuutekeleza hadi mwaka 2030, ambapo wafugaji watakuwa wamejengewa uwezo wa kujitegemea na kuendeleza shughuli zao bila kutegemea msaada wa wafadhili huku akisisitiza kuwa mafanikio ya mradi huo yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wafugaji na wadau wa maendeleo, hususan katika kuboresha miundombinu na huduma za kilimo na mifugo.

Akisoma taarifa ya mradi Mwenyekiti wa Bodi ya HAFEO Dkt. Amini Uroni,amesema lengo la mradi ni kuwajengea uwezo wafugaji wanaofuga kwa mfumo wa zero grazing kwa kuwapatia elimu ya lishe bora ya mifugo, uzalishaji wa malisho, utengenezaji wa silaji na matumizi ya teknolojia mbalimbali zitakazoongeza uzalishaji wa maziwa.


Aidha Dkt. Uroni amebainisha kuwa mradi huo unafadhiliwa na mashirika ya Global Agricultural Development Foundation (GAD) pamoja na Wilde Ganzen ya nchini Uholanzi, na kwa sasa unatekelezwa katika kata tatu za Halmashauri ya Wilaya ya Hai, huku kukiwa na matarajio ya kuupanua hadi kata zote 17 endapo ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na wafadhili utaendelea kuimarishwa.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo akiwemo Baraka Haji na Malika Abdi , wamesema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwani hapo awali walikuwa wakifuga kwa mazoea kutokana na ukosefu wa elimu ya ufugaji wa kisasa lakini baada ya mafunzo wameanza kutumia mbinu walizojifunza, ikiwemo utengenezaji wa silaji na kilimo cha malisho kwa teknolojia ya tumbukiza, hatua ambayo tayari imeanza kuongeza uzalishaji wa maziwa katika mifugo yao.