Boma Hai FM
Boma Hai FM
23 June 2026, 1:15 pm

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Omary Bomboko amesisitiza umuhimu wa mazoezi kwa afya na maendeleo ya jamii, huku akiwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za mapokezi ya Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kuwasili wilayani Hai Julai 3, 2026.
Na Juma Robert
Hai- Kilimanjaro
Wananchi wa Wilaya ya Hai wameungana katika mazoezi ya jogging yaliyoanzia katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, yakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Hassan Omary Bomboko, ambaye alikuwa miongoni mwa washiriki wa zoezi hilo.
Akizungumza mara baada ya mazoezi hayo Juni 20,2026 Bomboko amewahimiza wananchi kuendelea kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Jogging hiyo iliwakutanisha vijana, wanawake, wanaume pamoja na viongozi kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi, ambapo washiriki walifanya mazoezi kwa pamoja katika mazingira ya mshikamano na ushirikiano.
Aidha Bomboko ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo zitakazofanyika sambamba na mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2026 utakaowasili Wilayani Hai Julai 3, 2026.
Bomboko amesema Mwenge wa Uhuru ni chombo muhimu katika kuhamasisha uzalendo, umoja na maendeleo ya jamii, hivyo amewataka wananchi kujiandaa kuupokea kwa heshima kubwa na kushiriki kikamilifu katika shughuli zote zitakazoambatana na mbio hizo za kitaifa na kwamba mkesha utakuwa katika viwanja vya Snow View.
Kwa upande wake mrakibu mwandamizi wa polisi Oscar Joshua amewapongeza wananchi wa Wilaya ya Hai kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mazoezi hayo, akieleza kuwa ushiriki wao unaonyesha uelewa mkubwa kuhusu umuhimu wa afya pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na vyombo vya ulinzi na usalama.