Boma Hai FM
Boma Hai FM
3 August 2026, 12:21 pm

Wadau wa utalii na watu wenye ulemavu wameonyesha fursa na changamoto za walemavu wanazokutana nazo kwenye vivutio vya utalii pamoja na kuwapa fursa yakushiriki kwenye utalii wa ndani
Na Henry Keto, Hai-Kilimanjaro
Wadau mbalimbali wa utalii wa ndani wameiombwa kutangaza shughuli za utalii nchini kwa lengo la kuonyesha fursa, kujifunza na kufurahia vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya nchi ya Tanzania hasa kwa wale wenye nafasi za kutangaza vivutio ili kuongeza watalii kimataifa.
Wito huo umetolewa August 1,2026 na Diwani wa kata ya Masama Rundugai Simbano Aziz wakati wa shughuli ya kufanya utalii wa ndani kwa watu wenye ulemavu na Mahitaji maalumu wilaya ya Hai Yenye lengo la kuwapa fursa walemavu kushiriki kwenye vivutio vya utalii.
Simbano ambaye amemwakilisha mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amesema utalii wa ndani ni muhimu sana hasa katika zoezi la kufurahi pamoja na watu wenye ulemavu ambao wanapata kujifunza, kufurahi na kuona fursa kwenye utalii, mbali na hali zao walizonazo bado wanaweza kushiriki kwenye shughuli za utalii wa ndani na wenye tija kwao.
Ameongeza kuwa Changamoto wanazopitia watu wenye ulemavu katika maeneo ya utalii hasa maeneo ya chemka zinashughulikiwa na ujio wao unaendelea kuonyesha kipi chakuboresha zaidi ili wapate huduma nzuri kulingana na hali zao za ulemavu.
kwa upande wake moja ya waandaaji wa shughuli hiyo ya kufanya utalii wa ndani na watu wenye ulemavu msanii na mtengeneza maudhui mtandao Tegemeo Urassa maarufu kama Mwenyekiti amesema lengo la shughuli hiyo ni kufurahi pamoja na watu wenye ulemavu kwenye vivutio vya utalii pamoja kuonyesha fursa na Changamoto wanazopata watu wenye ulemavu katika maeneo ya utalii na kuonyesha jinsi gani watu wenye ulemavu wanaweza kupewa kipaumbele kwenye sekta hiyo muhimu.

Zoezi hilo limeungwa mkono na Viongozi mbalimbali wa serikali ya halmashauri ya wilaya ya Hai ambao wameshirikia katika safari hiyo na kujionea jinsi gani watu wenye ulemavu wanahitajii kupewa nafasi ili kuzitumia fursa na vipaumbele kwenye maeneo ya utalii hasa utalii wa ndani.
Afisa utalii wilaya ya Hai Casian Mwingira amepongeza waandaaji wa shughuli hiyo nakuwakaribisha waendelee kutembelea katika vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo wilaya ya Hai kwa lengo la kukuza utalii wa ndani na wenye tija kwa watanzania.
Nae Afisa ustawi wa jamii na mratibu wa watu wenye ulemavu wilaya ya Hai Maiko mahundi amesema kutembelea vivutio vya utalii kunatengeneza fursa,kujifunza na kujionea Changamoto wanazopitia watu wenye ulemavu ili serikali itambue na iweze kuboresha katika upande wa walemavu na kutoa huduma bora zaidi
Nao baadhi ya watu wenye ulemavu wameshukuru kwa wote walioshiriki kufanya jambo hilo jema kwako kwani imewafanya kujisikia vizuri na kufurahia vivutio vya utalii wa ndani hasa utalii wa kuogelea kwenye kivutio Cha Chemka Hot Spring.