Boma Hai FM
Boma Hai FM
22 July 2026, 10:39 am

Wananchi wa wilaya ya Hai wanatarajiwa kushiriki kongamano la siku tatu la mafunzo ya ujasiriamali litakalowajengea uwezo wa kuanzisha na kuendeleza biashara, kwa lengo la kuongeza fursa za ajira, kujiajiri na kukuza uchumi wa jamii.
Stanley Christian
Hai – Kilimanjaro
Wananchi wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wanatarajiwa kunufaika na kongamano la siku tatu la mafunzo ya ujasiriamali litakalofanyika kuanzia Julai 23 hadi 25, 2026 katika ukumbi wa Kilimanjaro Modern uliopo kata ya Muungano likiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kukuza shughuli za kiuchumi.
Akizungumza na Radio Boma Hai FM Julai 20 2026, diwani wa Kata ya Muungano ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai ambae ndie mdhamini wa Kongamano hilo Edmund Rutaraka, amesema mafunzo hayo yatawakutanisha wananchi kutoka kata mbalimbali za wilaya ya Hai ili kuwapa maarifa ya ujasiriamali yatakayowawezesha kuanzisha biashara na kunufaika na mikopo inayotolewa na halmashauri kupitia vikundi au mtu mmoja mmoja.
Rutaraka amesema washiriki watapatiwa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo sabuni za aina tofauti, mafuta ya kupaka, batiki, vikoi, vijora na keki na kwamba wawezeshaji wa mafunzo hayo watatoka katika Chuo cha Elimu kwa Wote kilichopo jijini Dar es Salaam.
Amesema waandaaji wanatarajia kushirikisha zaidi ya wajasiriamali 500 na amewahimiza wakazi wa Kata ya Muungano pamoja na kata nyingine za Wilaya ya Hai kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na fursa hiyo ya mafunzo.
Kwa upande wake, afisa biashara wa Wilaya ya Hai Christina Lyimo, amesema kongamano hilo litawajengea vijana uwezo wa kubuni na kuanzisha biashara, hatua itakayochangia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
“Ujasiriamali ni uthubutu wa mtu kufanya jambo lenye lengo la kujipatia kipato na ni elimu muhimu ambayo naamini itawakomboa vijana wengi kutoka katika changamoto ya ukosefu wa ajira na kuwapa uwezo wa kujiajiri,” amesema Lyimo.
Naye mjasiriamali wa Wilaya ya Hai, Paul Christopher Malongo, amesema anatarajia kupata maarifa na mbinu mpya zitakazomwezesha kuboresha shughuli zake za biashara na kujiongezea kipato na hatimaye kuajiri watu wengine.