Boma Hai FM

Jeni azikwa, Askofu Shoo ataka jamii kutatua changamoto kwa amani

10 October 2026, 9:01 am

Pichani ni baadhi ya waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Jeni Maloo Urassa anayedaiwa kufariki dunia kwa kupigwa risasi na mume wake( picha na Oliva Joel)

Askofu Fredrik Shoo ametoa wito huo wakati wa ibada ya mazishi ya Jeni Maloo Urassa wilayani Hai ,huku familia ya marehemu ikiomba waombolezaji kuepuka taarifa zisizothibitishwa na kueleza hatua zilizochukuliwa kuimarisha usalama wakati wa msiba.

Na Oliva Joel

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Askofu Fredrik Shoo, ameitaka jamii kudumisha amani na kuwashirikisha watu wanaowaamini wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali ili kusaidia kuepusha maamuzi yanayoweza kusababisha madhara.

Askofu Shoo ametoa wito huo Oktoba 9 2026, wakati wa ibada ya mazishi ya Jeni Maloo Urassa, anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na mume wake Laurence Kweka jijini Dar es Salaam ambapo Ibada hiyo imefanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Nkuu Kati, Kata ya Machame Mashariki wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Sauti ya Askofu Shoo

Kwa upande wake, msemaji wa familia ya Kweka Donald Kweka amesema familia hiyo imeumizwa na tukio hilo linalomhusisha ndugu yao, Laurent Kweka akieleza kuwa alidaiwa kumpiga risasi mke wake na baadaye kwenda kujisalimisha polisi.

Amesema Laurent alikuwa mtu mkimya na asiyezungumza sana, huku akibainisha kuwa hakuwahi kusikia taarifa za ndugu yao kufunguliwa kesi ya kumtishia mke wake.

Awali wakati ndugu, jamaa na marafiki wakimiminika nyumbani kwa familia ya Urassa katika Kijiji cha Nkuu Sinde Kata ya Machame Mashariki, familia hiyo iliwaomba waombolezaji kujiepusha na kusambaza au kujadili taarifa ambazo hawana uhakika nazo.

Sauti ya msemaji wa familia ya Kweka

Aidha familia hiyo imewaomba ndugu wa upande wa mume wa marehemu Laurence Kweka, kutofika nyumbani hapo wakati wa msiba, ikieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuepusha taharuki.

Sauti ya familia msemaji wa familia ya Jeni Urassa

Akizungumzia hali ya usalama nyumbani hapo, msemaji wa familia ya Urassa Judika Urassa, amesema ulinzi umeimarishwa huku taratibu nyingine za msiba zikiendelea kama kawaida.

Pichani ni baadhi ya waombolezaji wakiwa katika ibada ya mazishi ya Jeni Maloo Urassa( picha na Oliva Joel)

Inadaiwa kuwa Jeni Maloo Urassa  alifariki dunia kwa kupigwa risasi na mume wake Oktoba 1 2026, jijini Dar es Salaam na uchunguzi  wa tukio hilo bado unaendelea.