Orkonerei FM
Orkonerei FM
17 October 2026, 5:57 am

Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imezindua mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa unaolenga kuimarisha uratibu wa hatua za kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali baada ya majanga. Mpango huo umezingatia tathmini iliyobainisha vihatarishi mbalimbali, ikiwemo ukame, mafuriko na magonjwa ya milipuko.
Na Mwandishi Wetu
SIMANJIRO, Oktoba 16, 2026– Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Mhe. Kaleya Melita Mollel, amezitaka kamati za usimamizi wa maafa katika wilaya hiyo kutekeleza kikamilifu Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa ili kuimarisha maandalizi na uwezo wa kukabiliana na majanga.
Mollel ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa mpango huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, akisisitiza kuwa mpango huo unapaswa kutumika kama mwongozo wa vitendo badala ya kubaki kwenye nyaraka.
“Nitoe wito nendeni mkatekeleze yaliyomo kwenye mpango huu, mpango huu usibaki kwenye makaratasi kwani ni nyezo muhimu ya usimamizi wa maafa katika halmashauri yetu,” amesema Mollel.
Mpango huo unalenga kuweka miongozo na taratibu za kujiandaa na kukabiliana na maafa, hasa katika kipindi cha mvua za msimu, ili kupunguza athari zinazoweza kuikumba jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Kanali Selestine Masalamado, amesema mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia matokeo ya tathmini ya vihatarishi, uwezo wa wilaya kukabiliana na maafa na historia ya majanga yaliyowahi kutokea Simanjiro.
Masalamado amesema mchakato wa kuandaa mpango huo ulihusisha taasisi na wadau mbalimbali wa usimamizi wa maafa katika ngazi ya wilaya. Ameeleza kuwa mpango huo unatarajiwa kuwezesha uratibu wa shughuli za usimamizi wa maafa katika hatua zote za kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali.
“Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Idara ya Usimamizi wa Maafa, itaendelea kushirikiana nanyi, Wilaya ya Simanjiro katika shughuli za usimamizi wa maafa kwani usimamizi madhubuti wa maafa ni jukumu letu sote, kila mmoja ashiriki sasa na achukue hatua katika eneo lake, ili kulinda maisha na mali,” amesema Masalamado.
Ameongeza kuwa mpango huo ni hatua muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2004, toleo la mwaka 2025, pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022.

Tathmini ya vihatarishi na uwezo wa kukabiliana na maafa iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imebainisha kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na ukame, mafuriko, migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, moto, magonjwa ya milipuko kwa binadamu, mifugo na wanyamapori, upepo mkali pamoja na mimea vamizi.
Ofisi ya Waziri Mkuu imesema itaendelea kushirikiana na halmashauri hiyo katika kuimarisha usimamizi wa maafa, huku wadau na wananchi wakihimizwa kutekeleza wajibu wao katika kulinda maisha na mali dhidi ya majanga.