Orkonerei FM

Wafugaji Simanjiro washauriwa kuhifadhi malisho na kuchanja mifugo

4 June 2026, 2:19 pm

Wafugaji katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wameshauriwa kuchukua hatua za dharura za kuhifadhi malisho na kulinda vyanzo vya maji, ili kukabiliana na msimu wa kipupwe unaotarajiwa kuwa na baridi kali na ukavu mkubwa.

Na Isack Dickson

Rai hiyo imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa mkoa wa Manyara, ikisisitiza umuhimu wa wafugaji kushirikiana na wataalamu wa mifugo ili kuzuia milipuko ya magonjwa yanayoweza kuathiri mifugo yao.

Akizungumza na Orkonerei FM Radio, Meneja wa Hali ya Hewa Mkoa wa Manyara, Salma Amour Suleiman, amewataka wafugaji kutoipuuza tahadhari hii na badala yake waanze kujiandaa mapema kwa kuvuna na kuhifadhi malisho, pamoja na kusimamia vizuri vyanzo vya maji vilivyopo.

Meneja Salma amebainisha kuwa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa taarifa za hali ya hewa ndiyo siri ya kuongeza tija katika sekta ya mifugo na kilimo kwa sasa.

picha ya Meneja wa mamlaka ya hali ya hewa mkoa wa Manyara Salma Amour

Katika hatua nyingine, Salma ametoa wito kwa viongozi wa mila na vikundi vya wafugaji mkoani humo, kuhakikisha wanashirikiana bega kwa bega na maafisa ugani. Lengo likiwa ni kuendesha kampeni kabambe za chanjo na tiba kwa mifugo kabla ya athari za kipupwe kushamiri.

Amesema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imejipanga vizuri kutoa taarifa za utabiri kwa nyakati tofauti—ikiwemo taarifa za siku moja, siku tano, siku kumi, pamoja na taarifa za mwezi mzima—ili kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi.