Orkonerei FM
Orkonerei FM
7 May 2026, 11:55 am
Na Joyce Elius
Waandishi wa habari na watangazaji wa vipindi vya watoto, malezi, matunzo ya mtoto na familia nchini, wametakiwa kuwa vinara wa kuibua na kufuatilia habari zinazohusu vitendo vya kikatili vinavyofanywa katika jamii.
Wito huo umetolewa na wawezeshaji Victor Lugarabamu na Sabrina Majitaka, katika mafunzo ya siku tano yanayoendelea mkoani Dar es Salaam, yaliyolenga kuelimisha waandishi hao kuhusu wajibu wa wazazi na walezi katika malezi na matunzo ya familia.
Ikiwa ni siku ya nne ya mafunzo hayo, waandishi wa habari wamehimizwa kutumia kalamu na sauti zao kueleza dhana ya familia bora, ijengwe kupitia misingi ya kitamaduni ya malezi ya watoto kwa kuzingatia vipengele muhimu ikiwemo kumjali, kumlinda na kuzungumza na mtoto.
Wawezeshaji hao wameeleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuifikia jamii kwa haraka na kueleza changamoto za malezi, mila na desturi zenye madhara ambazo ni ndoa za utotoni, ukeketaji na ajira za watoto.

Changamoto nyingine walizozitaja ni suala la usawa wa jinsia katika malezi, kukithiri kwa ukatili wa kijinsia katika familia na utengano wa familia, mambo yanayotakiwa kuzungumzwa ili jamii iwe na uelewa juu ya madhara yanayojitokeza.
Mwezeshaji Sabrina Majitaka ameongeza kuwa jamii inatakiwa kutambua afya ya mtoto ni muhimu kwa kupata lishe, malezi na maendeleo kuanzia kipindi cha ujauzito hadi ujana.
Kwa kutambua hilo, wazazi na walezi, wanatakiwa kuendelea kuwajibika kwa watoto wao kwa kuwalea pamoja ili kupunguza na kutokomeza changamoto za malezi zilizopo katika jamii hasa baadhi ya kina Baba kuona jukumu la malezi ni la kina Mama, jambo ambalo si sahihi bali nafasi ya Baba ni kubwa katika malezi ya watoto.
Mafunzo hayo pia, yamegusia suala la lishe, ulinzi wa mtoto, umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa, kuwajali kina mama na watoto wenye ulemavu, kukabiliana na VVU na Ukimwi, na kuwajali vijana balehe.
Waandishi wa habari wanaonufaika na mafunzo hayo wamemshukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa kuwezesha mafunzo hayo ya siku tano ambayo yamesaidia kujenga uelewa wa masuala mbalimbali juu ya malezi na ulinzi wa mtoto.
