Orkonerei FM

Wafugaji na Chanjo ya UVICO 19.

8 November 2021, 2:15 pm

08.11.2021

Na Baraka David Ole Maika.

Jamii ya wafugaji wa Kimasai na Watanzania wote wametakiwa kujitokeza kupatiwa Chanjo ya UVICO 19 kwani chanjo hiyo ni salama na haina Madhara.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Dokta Godwin Mollel.

Akizungumza na Orkonerei FM Radio Mheshimiwa Dokta Mollel amesema kuwa Serikali iliposema isubiri kwanza haikumaanisha kuwa Chanjo hiyo haifai bali ilikuwa inajiridhisha.

Chanjo ya UVICO ni Salama – Mheshimiwa Dr Mollel.

Aidha Mheshimiwa Dokta Mollel amesema kuwa hakuna chochote kinachoingia Nchini pasipo Serikali kuifanyia Uchunguzi na kujiridhisha ili isije ikaleta Madhara kwa Watumiaji na Serikali inafanya hivyo kupitia Wataalam waliopo.

Serikali imejiridhisha kuwa Chanjo ya UVICO 19 ni salama.

Mheshimiwa Dr Mollel ameisihi Jamii ya Wafugaji hasa waliopo Vijijini kuachana na taarifa potofu zinazoenezwa kuwa Chanjo ya UVICO 19 ina Madhara kwa Afya ya Binadamu ikiwa ni pamoja na kuathiri Mfumo wa Uzazi na mtu kugeuka kuwa Zombi kwani ni Taarifa zisizo na ukweli.