Orkonerei FM

DC Serera aagiza TAKUKURU kuwachukulia hatua waliouza ardhi ya kijiji Loiborsiret

3 January 2024, 11:41 am

 “Jitihada hizi shirikishi zitachangia kuboresha usimamizi mzuri wa ardhi ya Vijiji na hatimaye itumike kwa maslahi ya Vijiji na Wananchi na si kwa Watu wachache wenye kujilimbikizia ardhi kinyemela bila kuiendeleza.” Dkt.Suleiman Serera ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram

Na Mwandishi wetu

Uongozi wa wilaya ya Simanjiro ukiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo Dkt. Suleiman Serera umemaliza mwaka 2023 kwa kuwasikiliza wananchi wa kijiji cha Loiborsiret waliowasilisha kero yao kubwa kuhusu ardhi ya kijiji hicho kutosimamiwa ipasavyo, ikiwemo eneo lililotengwa kwa ajili ya malisho kuvamiwa.

Akifungua kikao hicho cha kusikiliza kero hizo mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wlaya ya Simanjiro Gracian Makota amewataka wanakijiji kutoa kero zao pasi na kutumia lugha kali wala kushambuliana kwa namna yoyote ile, pia alitumia nafasi hiyo kujitambulisha.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Grancian Makota akizungumza katika mkutano huo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya Dkt.SERERA amesema kuwa kwakuwa upo mpango wa matumizi bora ya ardhi, basi ufuatwe na wale waliovamia eneo la malisho waondoke na Kuhusu maeneo yaliyouzwa kiholela, Jeshi la Polisi na TAKUKURU wameanza uchunguzi wa nyaraka za waliouziwa na waliouza ili kubaini kama kuna ukiukwaji wowote wa sharia hatua za kisheria zichukuliwe.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dkt.Suleiman Serera akizungumza katika mkutano wa kijiji cha Loiborsiret

Katika mkutano huo mbali na wananchi kupata nafasi ya kueleza kero zao pia walikuwa wameshika mabango baadhi yakielezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa viongozi wa kijiji hicho,wakiwatuhumu kuhusika na uuzwaji wa ardhi ya kijiji bila uamuzi wa mkutano mkuu wa kijiji.