Orkonerei FM

Serikali inaendelea kuwaboreshea mazingira ya kazi.

31 May 2022, 10:48 pm

 

Na mwandishi wetu.

Serikali kupitia wizara ya Afya, inaendelea na mkakati wa kuboresha miundombinu ya huduma za afya, unaoenda sambamba na ujenzi wa nyumba za watumishi wa Afya, ili wahudumu kuwa na makzi katika maeneo yao ya kazi pamoja na kuhakikisha wananchi hasa wa maeneo ya pembezoni wanapata huduma za afya kwa masaa 24.

Kupitia mkakati huo, wakazi wa kata ya Mwandeti na vitongoji vyake wamepata neema hiyo, ya kuongezewa miundombinu katika, iliyokuwa zahanati ya Mwandeti na kuwa kituo cha afya, sambamba na ujenzi wa nyumba ya wahudumu wa afya.

Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi ameweka wazi kuwa, halmashauri yake, ilipokea kiasi cha shilingi milioni 90, kutoka serikali kuu, ikiwa ni fedha za tozo za miamala ya simu, kwa ajili kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba ya watumishi wa kituo kipya cha afya Mwandeti, yenye sehemu ya kuishi watumishi watatu (3 in 1).

Aidha amefafanua kuwa, utekelezaji wa mradi huo, unaendelea vizuri, uko hatua za ukamilishaji, na unategemea kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa fedha, tayari kwa watumishi wa kituo hicho cha afya, kuanza kuishi na kuendelea na majukumu yao ya kuwahudumia wagonjwa, kama malengo ya serilali yanavyoainisha.

“Niseme tu, serikali ya awamu ya sita inatambua, kazi kubwa inayofanywa na wahudumu wa afya, inatambua mazingira yao ya kazi, ndio maana ina mkakati wa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya, pamoja na mazingira rafiki ya kuishi watumishi wa afya, hususan maneo ya pembezoni, ameneo ambayo yanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nyumba za kuishi” amefafanua Mkurugenzi Msumi.

Naye Mganga Mfawidhi Zahanati ya Mwandeti, Dkt. Aidan Martin amesema kuwa, ujenzi wa nyumba hizo za watumishi, umekuja kwa wakati sahihi kwa kuwa, uwepo wa nyumba za watumishi katika eneo la kazi, utawaongezea ari ya kufanya kazi, itaongeza weledi katika kutekeleza majukumu yao, ikiwa ni pamoja na utoaji na upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa kwa urahisi na kwa haraka wa muda wote wa siku.

“Daktari na wauguzi wanaposihi ndani ya eneo la kazi, inawarahisishia utekelezaji wa majukumu yao ya kazi, kuingia kazini kwa wakati, kutoa huduma kwa haraka hususani huduma za ’emergence’ hasa wakati wa usiku, lakini pia inaongeza wigo kwa wagonjwa kupata huduma kwa saa 24, kwa kuwa wauguzi wanapatikana eneo hilo kwa muda wote” amesema Dkt. Martin

Awali ujenzi wa nyumba hiyo ya watumsihi wa afya, umeenda samabamba na upanuzi wa miundombinu ya zahanati ya Mwandeti ili kuwa kituo cha afya, upanuzi uliohusisha ujenzi wa nyumba hiyo ya watumishi, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la mama na mtoto, maabara, jengo la X-ray na Laundry kwa gharama ya shilingi milioni 500.