Orkonerei FM

Ufunguzi wa soko la Alamayana kijiji cha Loswaki kata ya Terrat

7 March 2024, 4:54 pm

Viongozi na wananchi wakati wa ufunguzi wa soko la Alamayana kijiji cha Loswaki. Picha na Baraka Ole Maika.

Wananchi wa kijiji cha Loswaki kilichopo kata ya Terrat wilaya ya Simanjiro wameungana pamoja na wananchi wa vijiji vya jirani, wafanyabiashara, viongozi mbalimbali wa mila, chama na serikali katika ufunguzi wa soko la Alamayana katika kijiji cha Loswaki.

Na Baraka David Ole Maika.

Ufunguzi wa soko hilo umekwenda sambamba na ugawaji wa vizimba vya biashara kwa wafanyabiashara na wananchi wengine kwa ajili ya kufanyia shughuli zao za biashara siku ya soko na hata kwa siku zingine za wiki kabla ya siku ya soko.

Akizungumza na wananchi wakati wa ufunguzi wa soko hilo la Alamayana, diwani wa Kata ya Terrat ambaye alikuwa mgeni rasmi Mh Jackson Materi amesema kuwa ufunguzi wa soko hilo ni fursa kwa wananchi wa kata ya Terrat na wafanyabiashara na kuwasihi uongozi wa kijiji cha Loswaki kuonana na wafanyabiashara na kuwapatia fursa ya kuleta malori ya bidhaa katika soko hilo.

Sauti ya mheshimiwa Jackson Materi, diwani kata ya Terrat Simanjiro.
Mheshimiwa Jackson Materi, Diwani kata ya Terrat Somanjiro akizungumza na wananchi Sokoni Loswaki. Picha na Baraka Ole Maika.

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Loswaki Bw Mosses Michael Lukumay ametumia fursa ya ufunguzi wa soko hilo kuwaalika wafanyabiashara na wananchi wa vijiji na wilaya za jirani kuungana nao katika shughuli za biashara zote zilizo halali na maendeleo katika soko hilo la kijiji cha Loswaki.

Sauti ya Mosses Michael Lukumay, Mwenyekiti kijiji cha Loswaki.

Baadhi ya wananchi waliofika kushuhudia ufunguzi wa soko hilo wasema kuwa soko hilo ni fursa ya kipekee kwao kwani watakuwa wanapata huduma kwa karibu na kusihi uongozi wa kijiji cha Loswaki kuweka mazingira rafiki katika soko hilo na uwapatia wanawake kipaumbele katika maeneo ya kufanyia biashara.

Sauti za wananchi

Ufunguzi wa soko la Alamayana kijiji cha Loswaki ni muendelezo wa kufungua fursa za biashara na kukuza uchumi katika kata ya Terrat baada ya ufunguzi wa soko la Meibooroi katika kijiji cha Engonongoi hivyo kufanya kata ya Terrat kuwa na masoko matatu kwa wiki likiwepo soko kongwe la kijiji cha Terrat lililoanzishwa mwaka 1976.

Wachuuzi wakiwa soko la Alamayana kijiji cha Loswaki, Terrat Simanjiro. Picha na Baraka Ole Maika.