Orkonerei FM

Viongozi wa Mila na Chanjo ya UVIKO 19.

9 November 2021, 10:30 am

Terrat, Simanjiro 09.11.2021.

Na Baraka David Ole Maika.

Viongozi wa Mila na Chanjo ya UVIKO.

Viongozi wa Mila kutoka Jamii ya Kimasai Mkoa wa Manyara wamewataka Wananchi wa Jamii ya Kifugaji wa Kimaasai kujitokeza kupata Chanjo ya UVIKO 19 inayotolewa bila malipo kwani chanjo hiyo ni Salama na haina Madhara yeyote kwa Afya ya Binadamu.

Akizungumza na Orkonerei FM Radio kwa niaba ya Viongozi wa Mila Kiongozi wa Mila Alaiguanani Lesira Samburi kutoka Terrat Simanjiro amesema kuwa wao kama Viongozi wa Mila wanao wajibu wa kuhamasisha Jamii kutambua umuhimu wa kupatiwa Chanjo ya UVIKO 19.

Alaiguanani Lesira amesema kuwa kumekuwepo na taarifa potofu na zisizo na ukweli kuhusu Chanjo ya UVIKO 19 ikidaiwa kuwa chanjo hiyo ina Madhara kwa Afya ya Binadamu taarifa isiyo na Ukweli wowote kwani Serikali kupitia Wataalam wa Afya ilijiridhisha kuwa ni salama ndipo ikaanza kutumika.

Aidha Alaiguanani Lesira amesema kuwa yeye pamoja na Viongozi wengine wa Mila wamechanjwa mara tu baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Viongozi wengine wa serikali walipochanjwa na tangu wamechanja hawajapata Madhara yeyote ya Kiafya.

Naye Kiongozi wa Mila Alaiguanani Kimaath Ole Sima amesema kuwa huu ni wakati wa Jamii kutambua kuwa hakuna Kiongozi yeyote aliye na nia mbaya dhidi ya Wananchi wake hivyo serikali haina Mpango wa kuwadhuru wananchi wake kwa kutumia Chanjo ya UVIKO 19 ili ni Mpango wa Serikali kuwalinda Watanzania dhidi ya Maambukizi ya Virusi vya Korona nani kama Chanzo zingine zilizowahi kutolewa na Serikali.

Alaiguanani Ole Sima amesema kuwa ni vema serikali ikatoa elimu ya kutosha kwa Jamii juu ya umuhimu wa Chanjo ya UVIKO 19 na kusogeza huduma ya Chanjo kwa Wananchi tofauti na ilivyo sasa ambapo chanjo hiyo inatolewa katika Vituo vilivyobainishwa na Uongozi wa Wilaya ya Simanjiro.

Viongozi hao wa Mila kutoka Jamii ya Kimasai wamekutana katika Kijiji cha Terrat Wilayani Simanjiro kuzungumzia na kujadili mustaakbali wa maisha ya Jamii ya Wafugaji Wamaasai wakati huu wa UVIKO 19 na hali ya mienendo ya Vijana wa Kimaasai ambao wanatoka kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania kutafuta maisha.