Orkonerei FM

Kunywa damu mbichi hatari kwa afya-Utafiti

22 May 2026, 5:32 am

Na Dorcas Charles

Wafugaji katika Wilaya ya Simanjiro na maeneo mengine nchini wametakiwa kuzingatia usalama wa maziwa na kuacha kabisa utamaduni wa kutumia damu mbichi. Wito huo unafuatia matokeo ya uchunguzi wa sampuli za maziwa uliobaini uwepo wa viashiria vya magonjwa hatari kama vile brusela, kifua kikuu cha ng’ombe, pamoja na mabaki ya dawa yanayoweza kusababisha usugu wa vimelea mwilini.

Picha inamuonyesha Daktari Elibariki Mwakapeje kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) akiwa studio za Orkonerei Fm Radio………Picha na Isack Dickson

Akizungumza kupitia kipindi cha Amsha Amsha kinachorushwa na kituo cha redio cha Orkonerei FM, Daktari Elibariki Mwakapeje kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), alieleza kuwa shirika hilo lilifanya utafiti kwa kuchukua zaidi ya sampuli 4,000 nchini kote, huku sampuli 400 zikitoka katika kata sita na vijiji tisa vya wilaya ya Simanjiro kwa ajili ya vipimo vya maabara.

Kwa upande mwingine, Neema Moshi kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania alieleza umuhimu wa kufuata njia sahihi za uchemshaji wa maziwa ili kuua vimelea bila kuharibu ubora wake. Alishauri kuwa maziwa yasichemshwe kwa kutumia moto mkali kupitiliza hadi kuacha ukoko kwenye sufuria, bali yanapaswa kuchemshwa kwa kutumia mvuke au moto mdogo ili kulinda virutubisho vyake.

Picha inamuontesha Neema Moshi kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania akiwa studio za Orkonerei Fm Radio Picha na Isack Dickson

Naye Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt. Swaleeh Masaza, alifafanua hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa wanyama wanaogundulika kuwa na maambukizi. Alisisitiza kuwa ng’ombe wote wenye dalili za brusela wanapaswa kutengwa na kuondolewa kabisa kwenye kundi kwa ajili ya kuchinjwa, huku nyama yao ikiandaliwa kwa umakini wa hali ya juu ili kuzuia usambazaji wa vimelea vya brusela na kifua kikuu cha ng’ombe.

Picha inamuonyesha Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt. Swaleeh Masaza, akiwa studio za Orkonerei Fm Radio Picha na Isack Dickson