Orkonerei FM

RUWASA Simanjiro Kuondoa Kero ya Maji Kwenye Vitongoji 89 Ndani ya Miaka Miwili; Bei Mpya Kutangazwa Julai 2026

3 June 2026, 11:48 am

Na Isack Dickson

Vitongoji themanini na tisa ambavyo havijafikiwa na huduma ya maji safi na salama katika Wilaya ya Simanjiro, vinatarajiwa kuondolewa kwenye changamoto hiyo ndani ya miaka miwili ijayo, kufuatia mkakati madhubuti kutoka kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Hata hivyo, kukosekana kwa nishati hiyo kwenye vitongoji hivyo 89, kumesalia kuwa kero kubwa inayowalazimu wananchi kutumia muda mwingi kusaka maji badala ya kufanya kazi za uzalishaji.

Hatua hiyo inakuja wakati takwimu za hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu zikionyesha kuwa, upatikanaji wa maji vijijini ndani ya wilaya hiyo umefikia asilimia 77, ambapo zaidi ya wakazi laki moja na tisini na nne elfu wanapata huduma hiyo.

Meneja wa RUWASA wilayani Simanjiro, Johannes Martin, amesema kuwa Kupitia mpango huo ambao awamu yake ya kwanza tayari umeanza kutekelezwa, serikali inalenga kufikisha huduma hiyo katika maeneo yote yaliyosalia ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Licha ya mikakati hiyo ya serikali ya kusogeza miundombinu ya maji katika vitongoji vilivyosalia, changamoto nyingine inayowasumbua wananchi wa Wilaya ya Simanjiro ni pamoja na maombi ya kutaka kupunguziwa gharama za uunganishaji wa maji majumbani mwao pamoja na bei za huduma hiyo kwa ujumla.

Meneja Johanes ameeleza kuwa wananchi wenyewe ndio wenye dhamana ya kupanga bei hizo kwa kutoa maoni yao, ambapo kwa sasa katika mwezi huu wa Juni, mchakato wa kukusanya maoni hayo kote wilayani unaendelea kabla ya kuwasilishwa ngazi za juu kwa ajili ya maamuzi.

Wakati huo huo,Meneja wa RUWASA amewashauri wananchi watume maombi ya kufungiwa maji majumbani mwao ili kuepukana na adha ya kupanga foleni ndefu kwenye mabomba ya jumuiya na kuokoa muda wa kushiriki katika shughuli nyingine za kiuchumi.