Orkonerei FM

Wataalamu Wafichua Faida za Maziwa ya Kwanza ya Mama Baada ya Kujifungua

26 May 2026, 3:08 pm

Na Dorcas Charles

Wazazi Simanjiro na Maoneo yote Nchini  wamekumbushwa umuhimu wa kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo bila kuwapa kitu kingine chochote, ili kuwajengea kinga imara dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.

Picha kwa msaada wa Mtandao

Wito huo umetolewa na Mkunga Muuguzi kutoka Kituo cha Afya cha Tettar Simanjiro, Damas Sembwa, Kupitia kipindi cha Amsha Amsha cha Orkonerei Fm Radio ambapo amebainisha kuwa baada ya miezi hiyo sita ya mwanzo kukamilika, ndipo mzazi anaruhusiwa kuanza kumtambulishia mtoto vyakula vingine laini katika mwezi wa saba wa makuzi yake.

Akifafanua muundo wa maziwa ya mama, Sembwa ameeleza kuwa yana virutubisho vyote muhimu vinavyohitajika mwilini ikiwemo protini nyingi, sukari, na vitamini.

AIDHA DAMAS amewashauri  akina mama wanaonyonyesha kuzingatia utayari wa kisaikolojia na usafi wa miili yao kabla ya kuanza kuwanyonyesha watoto ili kuwalinda dhidi ya maambukizi ya vijidudu. Akibainisha kuwa ni muhimu kwa mama kuwa na utulivu wa akili wakati wa unyonyeshaji, huku akisisitiza umuhimu wa kusafisha maziwa kwa kitambaa safi kabla ya kumnyonyesha mtoto ili kuzuia magonjwa yanayoweza kuepukika.

Picha ya Mkunga Muuguzi Damas Sembwa akiwa studio za Orkonerei Fm Radio, Picha na Isack Dickson

Katika hatua nyingine, mtaalamu huyo amepiga vita dhana potofu iliyoota mizizi miongoni mwa baadhi ya jamii, ambapo akina mama wamekuwa wakikamua na kuyamwaga maziwa ya kwanza ya njano wakiamini kimakosa kuwa ni uchafu uliotakiwa kutoka.Damas, amefafanua kuwa maziwa hayo ya awali ni maalum yaliyosheheni hazina kubwa ya virutubisho vya protini, vitamini, na kingamwili muhimu sana kwa kiumbe kipya kilichozaliwa.