Orkonerei FM

Wanawake wafugaji Tanzania wanavyovunja vikwazo vya kilimo wakati tabianchi ikibadilika

22 October 2026, 8:35 am

Mkulima Ester Iddy akivuna mboga za majani kwa umakini kwa kutumia kisu kwenye bustani yake katika kijiji cha Terrat, Wilaya ya Simanjiro. Ester aliamua kujikita katika kilimo cha mboga cha umwagiliaji baada ya kilimo cha kutegemea mvua kushindwa kumpa kipato cha uhakika kufuatia mabadiliko ya hali ya hewa yasiyotabirika. (Picha: Isack Dickson)

NA ISACK DICKSON

Tunapofika katika bustani ya Ester Iddy, kijiji cha Terrat, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, tunamkuta akivuna mboga kwa ajili ya kujiandaa na siku ya soko la Alhamisi.

Siku za kawaida, anaweza kuuza mafungu 10 hadi 18 ya mchicha kwa majirani wanaotembelea bustani yake kununua mboga kwa ajili ya familia zao, pamoja na wafanyabiashara wanaonunua kwa jumla ili kuuza tena sokoni.

“Fungu moja la mchicha linauzwa shilingi 500, na mauzo ya siku yanaweza kufikia shilingi 20,000,” anasema.

Hata hivyo, siku za Alhamisi mahitaji huongezeka zaidi. Wafanyabiashara wanawake wanaofika bustanini wanaweza kufikia wanane, na kila mmoja hununua takribani mafungu 20.

Ester, mwenye umri wa miaka 39, anasema mapato ya uhakika kutokana na kuuza mboga humsaidia kukidhi mahitaji ya familia yake, yakiwemo kulipia ada za shule za watoto wake wawili.

Hapo awali alikuwa mkulima wa mahindi, lakini aliamua kulima mboga ili kupunguza gharama za kukodi ardhi na kuongeza mapato kupitia mazao yanayokomaa kwa muda mfupi, wakati mvua zikiwa hazitabiriki.

“Kukodi ekari moja kuligharimu shilingi 40,000 za Tanzania kwa msimu. Mvua zilipokuwa hazitabiriki, ungeweza kutumia fedha kuandaa shamba bila kujua kama mavuno yangeweza kufidia gharama hizo,” anasema.

Katika bustani aliyoanzisha miaka miwili iliyopita kwa kutumia akiba yake, hulima mchicha, spinachi na kabichi ya kichina kutegemea msimu.

Ester Iddy akihudumia bustani yake ya mboga iliyostawi vizuri katika kijiji cha Terrat. Kupitia kilimo cha mboga cha kiwango kidogo, Ester huingiza kipato cha kila siku kinachomwezesha kukidhi mahitaji ya familia na kugharamia elimu ya watoto wake. (Picha: Isack Dickson)

Alipata mbegu zake za kwanza za mboga kutoka Tanzania Conservation and Community Empowerment Initiative (TACCEI), shirika linalosaidia wanawake na jamii kuboresha hali zao za kiuchumi kupitia kilimo na biashara ndogondogo.

Bustani ya Ester ipo kwenye ardhi iliyotolewa na ILARAMATAK, shirika la kijamii ambalo pia husambaza maji kutoka kwenye kisima cha karibu kinachotumia nishati ya jua.

“Shirika linatoa ardhi na maji, huku mimi nikifanya kazi na kusimamia uzalishaji. Tunagawana mapato, kila upande ukipata takribani asilimia 50. Hakuna mkataba wa maandishi,” anasema.

Ameanza kuchukua hatua za kupanua bustani yake na kuanzisha umwagiliaji wa matone ili kupunguza matumizi ya maji. Kwa sasa, hutumia mabomba ya mpira kumwagilia mazao, njia ambayo anasema hutumia maji mengi. Kupanua uzalishaji kutahitaji pia miundombinu ya ziada ya kusambaza maji.

Yohana Meliyo Mollel, mtaalamu wa kilimo kutoka TACCEI, anasema umwagiliaji wa matone unaweza kuwasaidia wakulima kutumia maji kwa ufanisi zaidi.

“Kwa mfano, mtu akiwa na ndoo za lita 20 na akaweka mfumo rahisi wa umwagiliaji wa matone kwa kutumia mabomba madogo na membamba yaliyowekwa chini ya ardhi, anaweza kupunguza gharama za maji,” anasema.

Uzoefu wa Ester unatofautiana sana na wa Joyce Elius, anayelima mahindi, maharagwe na alizeti katika shamba la familia yao eneo hilo hilo.

Joyce hutegemea mvua, hali inayofanya shughuli zake za kilimo kuwa katika hatari ya kuathiriwa na mabadiliko ya muda na kiasi cha mvua.

“Katika msimu wa mwaka 2026, mvua za masika zilichelewa, kisha mvua kubwa zikanyesha kwa wakati mmoja. Hali hii ilifanya palizi kuwa ngumu na kuongeza matatizo ya wadudu waharibifu,” anasema.

Mwishowe, alivuna magunia 34 ya mahindi na magunia tisa ya maharagwe. Hata hivyo, anasema uzoefu wake wa awali unaonyesha jinsi uzalishaji unavyoweza kutofautiana kati ya misimu katika kilimo kinachotegemea mvua.

“Mwaka 2023, nililima ekari 10 na kuvuna magunia 30 ya mahindi kwa kila ekari. Mwaka huo hali ilikuwa nzuri,” anasema.

Hali ya Joyce inaakisi pengo la kijinsia katika upatikanaji wa kilimo cha umwagiliaji. Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) za mwaka 2025–2026, kati ya wakulima 15,022 waliokuwa katika vikundi 769 nchini na kupokea pampu za umwagiliaji, wanawake walikuwa 6,335 ikilinganishwa na wanaume 8,702.

Takwimu hizo zinaonyesha vikwazo vinavyowakabili wakulima wanawake katika kupata na kumiliki rasilimali muhimu za maji na ardhi zinazohitajika ili kuwa na uzalishaji wa kilimo ulio wa uhakika zaidi.

Mzee Godson Nduya, kiongozi wa mila wa jamii ya Kimaasai katika kijiji cha Terrat, Wilaya ya Simanjiro. Katika jamii yake, mitazamo ya kitamaduni kuhusu umiliki wa ardhi kwa wanawake inaendelea kubadilika, ingawa kupata fursa ya matumizi ya ardhi ya muda mrefu bado ni changamoto kubwa kwa wanawake wanaotaka kuwekeza katika kilimo. (Picha: Isack Dickson)

Godson Nduya, mzee wa kimila wa Kimaasai, anasema upatikanaji wa ardhi kwa wanawake umeimarika katika baadhi ya maeneo, lakini mitazamo ya kijamii kuhusu umiliki bado inaweza kuwa kikwazo.

Kwa maelezo yake, wanawake wanaweza kuruhusiwa kutumia ardhi kwa kilimo bila kuwa na haki sawa na za wamiliki wa ardhi.

Jane Mbuya, afisa kilimo wa Wilaya ya Simanjiro, anasema serikali inatoa elimu ya kilimo kwa wanawake wa eneo hilo kadiri wanavyozidi kujihusisha na kilimo cha mazao, shughuli ambayo kijadi ilifanywa zaidi na wanaume katika jamii ya wafugaji.

“Ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na ukame, tunatoa elimu ya kilimo kwa nyakati tofauti kuhusu mazao yanayoweza kustahimili hali kavu,” anasema Mbuya.

Elimu hiyo hutolewa kupitia mikutano ya vijiji na mashamba darasa.

Mbuya pia anasisitiza umuhimu wa kuwa na vyanzo mbalimbali vya mapato badala ya kutegemea shughuli moja pekee.

“Tunawaeleza kuwa wanaweza kupata kipato bila kutegemea tu kuuza mifugo sokoni au kuchinja wanyama kwa ajili ya kuuza. Wanaweza pia kuendesha biashara ndogondogo sambamba na ufugaji au kupata mapato kupitia kilimo cha mchanganyiko wa mazao,” anasema.

Wakati dunia ikiadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima, juhudi zaidi zinahitajika kuwafikia wanawake kama Ester na Joyce. Ingawa programu za serikali kama Building a Better Tomorrow (BBT) zinalenga kuwawezesha vijana na wanawake katika kilimo, utekelezaji wake bado unakabiliwa na changamoto za kiufundi.

Utafiti wa mwaka 2024 uliochunguza maoni ya vijana kuhusu programu ya BBT mkoani Manyara ulibaini kuwa, ingawa vijana wengi waliiona kama fursa ya ajira, takribani asilimia 40 hawakuwa na ujuzi wa kiufundi katika kilimo.

Takwimu hizi zinaonyesha umuhimu wa mipango kama Gender Equality and Inclusion–Gender Accelerator inayoongozwa na CGIAR. Mpango huo unalenga kuweka usawa wa kijinsia katikati ya utafiti na maendeleo ya kilimo ili wanawake wanufaike kwa usawa na mabadiliko katika sekta hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya CGIAR GENDER Accelerator, uzoefu wa wanawake hawa unaonyesha kuwa kuwaunga mkono wakulima wanawake kunahitaji zaidi ya kuwahamasisha kulima mazao. Kunahitajika huduma za ugani zinazofikika, teknolojia yenye gharama nafuu, upatikanaji wa uhakika wa maji na ardhi, pamoja na takwimu za kuaminika zitakazowasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi.

Changamoto wanazokabiliana nazo zinaendana na onyo la Ismahane Elouafi, mkurugenzi mtendaji mkuu wa CGIAR.

“Hatuwezi kulisha dunia yetu ya baadaye bila kuwajumuisha wanawake katika mifumo yetu ya chakula. Maamuzi tutakayofanya katika miaka ijayo yataamua kama mifumo yetu ya chakula, ardhi na maji itakuwa na usawa zaidi au itaendelea kuwa isiyo sawa, na kama itakuwa imara zaidi au dhaifu zaidi,” anasema.

Hatua hizi ni muhimu si tu kwa maisha na kipato cha wakulima mmoja mmoja, bali pia katika kutekeleza mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama wake, ikiwemo Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW).

Mikutano ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo Mkutano wa Nchi Wanachama (COP), inapaswa pia kuzingatia mahitaji halisi ya wakulima wanawake kama Ester na Joyce. Hii inamaanisha kuhakikisha wanapata maji, ardhi na nishati safi, huku mifumo ya chakula ikiimarishwa ili iweze kukabiliana na mishtuko na mabadiliko.

Nicoline de Haan, mkurugenzi wa CGIAR GENDER Accelerator, anatoa mwongozo wa kufikia malengo hayo: “Kuwekeza kwa wanawake si kama vibarua bali kama viongozi ndiyo njia pekee ya kufungua uwezo kamili wa mifumo yetu ya chakula, ardhi na maji.”

Salma Amour, meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) mkoani Manyara, anasema uchambuzi wa takwimu za mamlaka hiyo unaonyesha kuwa mvua za mwaka zimepungua kwa takribani milimita moja hadi sita kwa mwaka katika baadhi ya maeneo, yakiwemo Simanjiro na sehemu za Kilimanjaro. Baadhi ya vituo vya hali ya hewa vimerekodi upungufu wa milimita 20 hadi 45 kwa kila muongo.

Kwa kiwango cha kitaifa, takwimu za TMA zinaonyesha kuwa mvua zilipungua kwa wastani wa milimita 45.9 kwa kila muongo kati ya mwaka 1950 na 2020.

Kupungua kwa mvua kuna athari za moja kwa moja kwa wanawake. Kwa mujibu wa ripoti mpya ya CGIAR GENDER Accelerator iliyotolewa Oktoba 15, 2026, kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake wa Vijijini, mabadiliko ya tabianchi yanatarajiwa kupunguza zaidi upatikanaji wa maji. Hali hiyo inaweza kuongeza kwa asilimia 30 muda ambao wanawake hutumia kutafuta na kuchota maji ifikapo mwaka 2050.

Makala hii imechapishwa kwa msaada wa The Media for Environment, Science, Health and Agriculture (MESHA).