Kahama FM
Kahama FM
26 October 2026, 1:05 am

‘‘Wananchi wa kata ya Busoka wataka barabara na eneo rasmi la soko katika Mpango Kabambe wa Kidigitali kahama’’
Wananchi wa Mtaa wa Busoka katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, wameiomba Serikali kuweka utaratibu utakaohakikisha wamiliki wa ardhi wanalindwa na kunufaika na mali zao wakati wa utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Kidijitali wa kupanga mji wa Kahama kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2050.
Wananchi hao wamesema ni muhimu Serikali kuweka wazi utaratibu wa tathmini na fidia kwa maeneo yatakayoguswa na utekelezaji wa mpango huo, ikiwemo yale yatakayotengwa kwa ajili ya masoko, vituo vya mabasi na miundombinu mingine ya maendeleo.
Akizungumza katika kikao cha Kupanga Kahama ya Baadaye, mkazi wa Busoka, Isaya Wapi, amesema wananchi wanahitaji uhakika kwamba upangaji upya wa mji hautawaingiza katika umasikini kutokana na kupoteza thamani ya mali zao.

Amesema baadhi ya wananchi wanaweza kumiliki viwanja vyenye thamani kubwa, lakini wakati wa tathmini kwa ajili ya fidia wakapangiwa thamani ndogo isiyolingana na thamani halisi ya maeneo yao.
Aidha, wananchi hao wameiomba Serikali kuipa kipaumbele mipango ya ujenzi na upangaji wa miundombinu ya barabara ili kuhakikisha mji unakuwa na mpangilio mzuri na unaokidhi mahitaji ya wakazi.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji wa kata Busoka Irene Olotu, amesema kutengwa kwa eneo rasmi la soko kutarahisisha shughuli za biashara na kuwapa wananchi mazingira bora ya kufanya shughuli zao za kiuchumi.

Naye, Mtaalamu wa Maendeleo ya Jamii na Usalama kutoka kampuni ya Urban Solution, Novatus Kaijage, amesisitiza umuhimu wa kupanga maeneo ya masoko kwa kuzingatia ongezeko la watu na mahitaji ya biashara kwa miaka ijayo.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Zacharia Shila, amesema Mpango Kabambe haupaswi kuishia katika kupanga maeneo ya ujenzi pekee, bali unapaswa kuzingatia pia uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira safi na salama.
Hata hivyo, ushirikiano kati ya wataalamu na wananchi umeelezwa kuwa muhimu katika kuhakikisha Mpango Kabambe unatekelezeka na kuleta maendeleo yanayozingatia mahitaji ya jamii, huku ukilinda haki za wananchi na kuhakikisha matumizi endelevu ya ardhi na mazingira.