Kahama FM
Kahama FM
30 June 2026, 12:23 pm

”kuanzia sasa ni marufuku mgeni yeyote kuingia kwenye nyumba yeyote ya kupanga bila ya utambuzi”
Wamiliki wa nyumba za kupanga na kulala wageni(Guest House) wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wamepigwa marufuku kupangisha ama kupokea mgeni katika nyumba za kulala wageni bila ya utambulisho wa kuwatambua.
Agizo hilo limetolewa leo na mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda, katika kikao na wamilili wa nyumba za kulala wageni na nyumba za kupangisha, ambapo amesema kwa nyumba za kulala wageni kuanzia sasa wanapaswa wageni kuwa na kitambulisho cha NIDA au hati ya kusafiria.
Aidha, Nkinda ameongeza kuwa kwa wale ambayo mpaka sasa hawana kitambulisho cha Nida ama hatari ya kusafiria wanapaswa kuwa na barua ya utambulisho kutoka kwa mwenyekiti mtaa/kijiji ama mtendaji wa kata/kijiji.

Nao, baadhi wa wamiliki wa nyumba za kulala wageni wilayani Kahama, wakizungumza kwa nyakati tofauti akiwemo Deogratias Joseph na Magdarena Charles, wamesema kuwa wamepokea agizo hilo na wanakwenda kulitekeleza, huku wakiomba baadhi ya watu kupatiwa vitambulisho vya DINA kwa ambapo mpaka sasa hawana ili kuondoa usumbufu.

Kwa upande wake, afisa Usajili Mamlaka wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wilaya ya Kahama Silieli Mchomvu amesema kuwa wameendelea kugawa vitambulisho vya DINA kwa kila kata wilayani humo kwa ambao mpaka sasa hawajapata, huku akiomba wananchi kutoa ushirikiano ili zoezi hilo likamilike kwa wakati.