Kahama FM

KUWASA yamlipisha Faini ya Shilingi Milioni mbili Samweli Samson Mwita

July 11, 2023, 5:52 pm

Viongozi mbalimbali wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira ( KUWASA )wakikagua baadhi ya miundombinu iliyoharibiwa picha na William Bundala

Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Kahama (KUWASA) imeanzisha kampeni ya kuwabaini watu wanaohujumu mamlaka hiyo ndani ya manispaa ya Kahama kwa kushirikiana na wananchi

Na William Bundala

Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Wilayani Kahama mkoani Shinyanga (KUWASA) Imemlipisha Faini ya Shilingi Milioni mbili bwana Samweli Samson Mwita mkazi wa Nyakato kata ya Nyasubi kwa kosa la kuhujumu mamlaka hiyo kwa kujiunganishia maji na kumwagilia bustani ya mbogamboga.

Akizungumza na Kahama Fm Afisa uhusiano wa mamlaka hiyo John Mkama amesema kuwa mteja wao bwana Samweli mwita amekubali kutenda kosa hilo na kwamba amekubali kulipa kiasi hicho cha fedha kwa awamu mbili ambapo katika awamu ya kwanza amelipa shilingi Milioni moja.

Sambamba na hayo Mkama amesema kuwa Mamlaka imeondoa mfumo mzima wa huduma ya maji kwa mteja huyo na kwamba pindi atakapomaliza kulipa faini hiyo atatakiwa kuanza upya kuomba kuunganishiwa huduma hiyo.

Katika hatua nyingine Mkama amesema kuwa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira kahama (KUWASA) imemkamata bwana Hamis Omary mkazi wa Mwime kata ya Mwendakulima kwa tuhuma za kujiunganishia maji kwa kuchepusha mfumo (bypass) nyumbani kwake.

Baadhi ya bomba likionesha namna ambavyo bw. Hamis Omar anaunganisha huduma ya maji

Mkama ametoa wito kwa wananchi wilayani Kahama kuendelea kushirikiana na mamlaka ya maji Kutoa taarifa za siri zitakazowezesha kuwabaini watu wanaohujumu mamlaka.

Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Kahama (KUWASA) imeanzisha kampeni ya kuwabaini watu wanaohujumu mamlaka hiyo ndani ya manispaa ya Kahama kwa kushirikiana na wananchi wanaotoa taarifa za siri.