Kahama FM

NAOT yawanoa wanahabari Shinyanga

June 28, 2023, 2:46 pm

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (National Audit Office of Tanzania – NAOT) imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club – SPC) ambapo waandishi wa habari wamejengewa uwezo kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo nafasi ya vyombo vya habari katika kuandika ripoti za ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aina za ripoti za ukaguzi pamoja na sheria , taratibu na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.

Akifungua mafunzo hayo Juni 28, 2023 kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere, Msaidizi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (AAG), Anna Massanja amesema vyombo vya habari ni miongoni mwa wadau muhimu wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi vikiwa na jukumu la kuandika habari, makala na uchambuzi kuhusu ripoti za ukaguzi wa CAG na taarifa za jumla za CAG, kuibua masuala muhimu ambayo yanaweza kuchunguzwa na ambayo yanaweza kupelekea ukaguzi maalum.

Amesema pia vyombo vya habari hutoa taarifa kuhusiana na hatua zilizochukuliwa na serikali katika kutekeleza mapendekezo ya CAG pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu majukumu ya CAG ili kuendeleza uwajibikaji nchini.

Msaidizi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (AAG), Anna Massanja 

“Tunatambua na kuheshimu mchango mkubwa wa waandishi wa habari katika kuelimisha umma, jambo ambalo limesababisha jamii kuendelea kufahamu na kutambua umuhimu wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi”, amesema Massanja.

“Hii siyo mara ya kwanza Ofisi ya Taifa ya ukaguzi kufanya mafunzo ya aina hii kwa waandishi habari, kwani kwa muda mrefu tumekuwa tukiendesha mafunzo ya aina mbalimbali kwa wahariri na waandishi wa habari kutoka maeneo mengine na mafunzo haya yatakuwa endelevu,”ameongeza Massanja.

Aidha amewahimiza waandishi wa habari kuwa na uelewa mkubwa wa masuala ya fedha za umma na kujifunza kuhusu mifumo ya bajeti, taratibu za manunuzi na sheria zinazosimamia matumizi ya fedha za umma, ujuzi ambao utawawezesha kufanya uchambuzi bora na kutoa taarifa sahihi kwa umma.

Naye mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi habari kutambua kwa upana shughuli za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa nje wa hesabu za serikali, ili kuisaidia jamii kupata uelewa kupitia habari na kufuatilia rasilimali zao kwa ajili ya maendeleo.