Kahama FM
Kahama FM
24 June 2026, 3:32 pm

Wadau wa maji katika Manispaa ya Kahama wameiomba Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) kuboresha huduma ya magari ya kusomba maji taka pamoja na kuongeza kasi ya ukarabati wa mabomba yanayopasuka mitaani mara baada ya taarifa kutolewa na wananchi.

Wadau hao wametoa maoni hayo leo wakati wa kikao cha wadau kilichojadili mipango ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo, wakisema maboresho hayo yataongeza ufanisi wa huduma na kupunguza kero kwa wananchi.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa KUWASA, John Mkama, amesema mamlaka hiyo inaendelea na ujenzi wa mifumo rasmi ya majitaka ili kuboresha usafi wa mazingira na huduma kwa wananchi.

Aidha, amewataka Maafisa Maendeleo wa Kata pamoja na wenyeviti wa mitaa kushirikiana katika kukomesha tabia ya baadhi ya wananchi kutiririsha maji taka ovyo pindi mashimo ya vyoo yanapojaa, akieleza kuwa hali hiyo ni hatari kwa afya ya jamii na mazingira.
Akihitimisha, Mkama amesema KUWASA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma za maji safi na usafi wa mazingira zinaimarika na kukidhi mahitaji ya wananchi wa Manispaa ya Kahama.