Kahama FM

RC Mhita aiomba ofisi ya CAG kufanya ukaguzi maalum Msalala

9 July 2026, 10:37 am

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita (Picha na Sebastian Mnakaya)

‘‘Hatua hiyo ni muhimu ili kubaini ukweli kuhusu matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha uwajibikaji unazingatiwa katika usimamizi wa rasilimali za wananchi’’

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameiomba Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu katika Halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama, ili kubaini mwenendo wa matumizi ya fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ametoa ombi hilo leo wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Msalala kilicholenga kujadili na kutoa majibu kuhusu hoja zilizobainishwa na CAG.

Mhita amesema hatua hiyo ni muhimu ili kubaini ukweli kuhusu matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha uwajibikaji unazingatiwa katika usimamizi wa rasilimali za wananchi.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Mibako Mabubu, ameahidi kushirikiana na Kamati ya Fedha kushughulikia changamoto zilizobainishwa kwenye ripoti ya CAG ili kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kuzuia hali hiyo kujirudia katika miaka ijayo.

Sauti ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Mibako Mabubu

Halmashauri ya Msalala ndiyo pekee kati ya halmashauri sita za Mkoa wa Shinyanga iliyopata hati yenye mashaka, jambo alilosema haliridhishi kutokana na jitihada za Serikali katika kupeleka fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.