Kahama FM
Kahama FM
29 June 2026, 6:25 pm

‘‘Tumieni elimu mlioyoipata kuboresha na kuongeza thamani bidhaa zenu na kuongeza vipato vyenu’’
Wajasiriamali wa kata ya Nyahanga Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wametakiwa kutumia elimu ya ujasiriamali walioipata wakaifanyie kazi kwa vitendo ili kuimarisha biashara zao na kuongeza vipata vyao kutokana na shughuli wanazozifanya.
Kauli imetolewa na diwani wa kata ya Nyahanga Josephina Kilimba wakati wa kufunga mafunzo ya ujasiriamali, aliyotolewa na Taasisi ya Star Enterpreneur General kwa kushirikiana na diwani Kilimba, ambapo amesema kuwa baada ya mafunzo hayo wanapaswa kwenda kuyafanyia kazi ili kuboresha biashara na kupata masoko ya uhakika

Aidha, Kilimba amesema kuwa kupitia mafunzo hayo itawasaidia wajasiliamali kukua kiuchumi na kuongeza thamani ya bidhaa wanazozitengeneza kwa kutumia teknelojia ya kisasa na inayoendana na wakati.

Kwa upande wake, katibu wa wajasiriamali wilaya ya Kahama Devother Herry, amewashauri wajasiriamali hao wasikate tamaa kutokana na changamoto mbalimbali wanazokutanazo, huku akiwataka kuchamkia fursa ya mikopo inayotolewa na serikali yenye masharti rafiki.

Nao, baadhi ya wajasiriamali waliopata mafunzo hayo wakizungumza kwa nyakati tofauti, akiwemo Daud Sonda na Veronica James, wameishukuru serikali kupitia diwani wa kata ya Nyahanga kwa kupatiwa mafunzo hayo bure ambayo yatakwenda kuwasaidia katika shughuli za kiuchumi hasa katika kuboresha biashara zao.
Zaidi ya wajasiriamali 75 wa kata ya Nyahanga wamepatiwa mafunzo ya siku 5 ya ujaliamali bure, huku yakilenga kuwapatia njia bora ya utengenezaji wa Batic na bidhaa za usafi, vipodozi, kilimo biashara na masoko.