Kahama FM
Kahama FM
28 April 2026, 4:14 pm

Mkurugenzi wa Huduma za Leseni wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi (Sebastian Mnakaya)
Wakaguzi Wakuu wa Migodi pamoja na wachimbaji wadogo nchini wamesisitizwa umuhimu wa kuimarisha usalama kazini, kulinda mazingira na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Na Sebastian Mnakaya
Wito huo umetolewa wilayani Kahama, mkoani Shinyanga na Mkurugenzi wa Huduma za Leseni wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, alipokuwa akifungua mafunzo kwa mameneja na Wakaguzi Wakuu wa Migodi ya uchimbaji mdogo kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhandisi Swedi amesema Wakaguzi Wakuu wa Migodi wanapaswa kupewa ushirikiano na mazingira wezeshi ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu, hatua itakayosaidia kuzuia ajali migodini, kulinda afya za wachimbaji na kuhifadhi mazingira yanayozunguka maeneo ya uchimbaji.

Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema Wakaguzi Wakuu wa Migodi wanapaswa kuwasilisha taarifa za ukaguzi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kubaini mapema vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali na kuchukua hatua za kinga kwa wakati.

Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa migodi mbalimbali kutokea mkoa wa Shinyanga wakizungumza kwa nyakati tofauti weishukuru Tume ya Madini kwa kuanda mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kwa kiasi kubwa kupunguza ajali za migodini.
Mafunzo hayo yanawakutanisha washiriki kutoka mikoa ya kimadini ya Kahama, Mbogwe na Shinyanga yakilenga kuimarisha uelewa wa kitaalam, usimamizi bora wa migodi, uzingatiaji wa sheria na kanuni pamoja na kukuza uchimbaji salama na endelevu.