Kahama FM
Kahama FM
22 July 2026, 1:51 am

‘‘Wafanyabiashara tumieni mfumo wa IDRAS kulipa kodi na kujua taarifa mbalimbal zinazopatikana kupitia mfumo huo’’
Na Mwandishi wetu
Wafanyabiashara wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kutumia mfumo jumuishi wa usimamizi wa kodi wa ndani (IDRAS) ili kurahisha ulipaji wa kodi kwa urahisi, huku mfumo huo ukihitaji mtumiaji kulipa kodi kwa wakati.
Wito huo umetolewa na meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa mkoa wa kikodi Kahama Wisaka Kamwamu, wakati akizungumza na Kahama Fm ambapo amesema mfumo huo una huduma zote ambazo unaweza kuzifanya nyumbani bila ya kufika ofisi za TRA.

Aidha, Kamwamu amesema kuwa mfumo huo mpya wa kidigitali unajumuisha mifumo yote ya TRA, huku ukiwasaidia wafanyabiashara hao kujua huduma mbalimbali kupitia mfumo huo.
Katika hatua nyingine, Kamwamu amewataka baadhi ya wafanyabiashara kuacha tabia ya kukwepa kulipa kodi na badala yake walipe kwa hiari bila ya kusukumwa kwa ajili maendelea ya nchi, huku akimtaka mfanyabiashara atakayepata changamoto aziwasilishe ofisini TRA.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa wafanyabiashara wilaya ya Kahama Charles Machali amesema kuwa kwa sasa TRA wana mifumo mizuri na bora ya ulipaji wa kodi na pia imepunguza mianya mingi ya ukwepaji wa kulipa kodi kwa wafanyabiashara.
Nao, baadhi ya wafanyabiashara wa Manispaa ya Kahama akiwemo Boni Fantaleo na Simon Mtaamuli wamesema kuwa wameendelea kujitahidi kulipa kodi kwa hiari pamoja na kutoa risiti ili kuondokana na biashara za magendo pamoja na kulichangia taifa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) kwa mkoa wa kikodi Kahama ulikusanya mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026 shilingi bilioni 32.2, huku kwa mwaka wa fedha 2026/2027 wakiwa na malengo ya kukusanya shilingi bilioni 50.4