Kahama FM
Kahama FM
23 August 2026, 6:43 pm

Mradi wa ufugaji nyuki unaofanywa na kikundi cha Tukwikondele katika Kijiji cha Buyange, Kata ya Bugalama, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, umetajwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi, huku ukichochea uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2015 kikiwa na mizinga saba pekee, hali iliyofanya uzalishaji wa asali kuwa mdogo hata hivyo, baada ya kupata uwezeshaji wa kifedha na kujengewa uwezo katika ufugaji nyuki wa kisasa, kikundi hicho kimeweza kuongeza uzalishaji na sasa kinazalisha zaidi ya lita 200 za asali kwa mwaka.

Mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na changamoto nyingine zinazotokana na uharibifu wa mazingira, ambazo zimekuwa na athari kwa maisha na shughuli za kiuchumi za wananchi.
Akizungumza baada ya kutembelea na kukagua shughuli za ufugaji nyuki na upandaji miti zinazofanywa na kikundi hicho, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amesema mradi huo umeonyesha namna uhifadhi wa mazingira unavyoweza kwenda sambamba na maendeleo ya kiuchumi.

Mwang’onda amewahimiza wananchi kuendelea kupanda miti, kutunza mazingira yanayowazunguka na kulinda vyanzo vya maji kwa kuhakikisha wanapanda miti rafiki kwa mazingira.

Kwa upande wake, Kiongozi katika idara ya mahusiano na jamii kutoka mgodi wa barick Bulya Zuwena Semtondo amekita kikundi hicho kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti na kuendelea na ufugaji wa nyuki.
Kwa sasa, kikundi hicho huzalisha zaidi ya lita 200 za asali kwa mwaka, ambapo mradi huo unaonyesha kuwa ufugaji nyuki na uhifadhi wa mazingira vinaweza kwenda pamoja, kwani uwepo wa miti na mazingira salama kwa nyuki huongeza uzalishaji wa asali, huku upandaji miti ukisaidia kulinda bioanuwai, vyanzo vya maji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.