Kahama FM
Kahama FM
18 September 2026, 1:39 am

Diwani wa Kata ya Nyahanga katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Josephina Kilimba, amewapongeza vijana wa kata hiyo kwa kuonyesha uwezo na vipaji vyao katika michuano ya mpira wa miguu.
Na mwandishi wetu
Vijana waliofanya vizuri katika michuano hiyo wamepata nafasi ya kuchaguliwa kuiwakilisha Kata ya Nyahanga katika mashindano ya Ngayiwa Cup, yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni, huku vijana hao wakipatiwa zaidi ya shilingi laki tatu na ishirini kama kuwapa motisha kuendea kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Akizungumza baada ya mchezo wa fainali uliowakutanisha Nyahanga Academ na Hongwa, ambapo Nyahanga Academ ilishinda kwa mabao matano kwa sifuri, Kilimba amesema michuano hiyo imeibua vijana wengi wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kucheza soka.
Amesema jumla ya vijana 25 wamechaguliwa kuunda timu itakayoenda kuiwakilisha Kata ya Nyahanga katika mashindano hayo, baada ya kuchaguliwa kutoka katika timu tano zilizoshiriki michuano ya kata hiyo, huku akiwataka vijana hao kutumia fursa hiyo kuonyesha uwezo wao na kuiwakilisha vyema Kata ya Nyahanga katika mashindano ya Ngayiwa Cup.

Mratibu wa michuano hiyo ya Ngayiwa Cup, Mikday Herry, amesema kuwa vijana waliopata fursa ya kucheza michuano hiyo wanatakiwa kujitahidi kuonyesha vipaji vyao ambapo zitaweza kuwapeleka mbali katika mchezo wa mpira wa miguu, huku akimpongeza diwani wa kata hiyo kwa kutengeneza mazingira rafiki kwa vijana kuonyesha vipaji vyao.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Nyahanga Lucas Matanyange, amewataka vijana waliochaguliwa katika timu ya kata kuwa na bidii na nidhamu pamoja na kuzingatia muda wa mazoezi ili waweze kuwa washindi ya michuano hiyo.
Mbunge wa jimbo la Kahama mjini Benjamini Ngayiwa ameandaa michuano hiyo ya mpira wa miguu itakayoshirikisha kata 20 katika jimbo hilo, huku mshindi wa kwanza katika michuano hiyo kuzawadiwa shilingi milioni tano.
