Kahama FM
Kahama FM
22 August 2026, 1:43 pm

‘‘Endeleeni kusajili vikundi na kutumia katika zabuni mtakazokuwa mnatangaza ili nao wawe sehemu ya wanufaika’’
Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imefanikiwa kusajili jumla ya vikundi 326 vya makundi maalum katika Mfumo wa Manunuzi ya Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST), sawa na 217% ya lengo lililowekwa, huku ikifanikiwa pia kutoa zabuni kwa vikundi hivyo.
Mafanikio hayo yameifanya Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kutunukiwa tuzo na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kuonesha ufanisi mkubwa katika zoezi la kusajili na kutoa kazi (tender) kwa makundi maalum kupitia mfumo wa NeST.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu amekabidhiwa tuzo hiyo na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Mwang’onda, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Serikali katika ziara ya Mwenge huo.

Akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, afisa maendeleo ya jamii wa Manispaa hiyo, Mbwana Karata amesema Halmashauri hiyo imetenga jumla ya Shilingi 1,943,353,500, sawa na 30% ya manunuzi ya Serikali, kwa ajili ya kuwawezesha makundi maalum kunufaika na fursa za zabuni.

Aidha, Mbwana amesema kuwa kutambuliwa na PPRA kupitia tuzo hiyo ni ishara ya ushirikiano uliopo katika utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri imefanikiwa kuwa na matokeo chanya, huku akiwapongeza watumishi na viongozi wote walioshiriki katika kufanikisha zoezi hilo.
Hata hivyo, Mafanikio hayo yamepatikana katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya mfumo wa NeST katika ununuzi wa umma, kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na ushiriki wa makundi mbalimbali katika fursa za zabuni za Serikali.
