Kahama FM

Sindano; Chakula shuleni chatajwa kuwa muhimu katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi

24 September 2026, 1:32 am

Mgeni rasmi ambaye ni pia diwani wa kata ya Nyihogo Sindano William akizungumza na wanafunzi pamoja na wazazi katika mahafali 2 ya shule ya sekondari Anderson Msumba ( Picha na Sebastiani Mnakaya)

‘‘Wazazi Kahama Wahimizwa Kushirikiana Kuhakikisha Wanafunzi Wanapata Chakula Shuleni’’

Wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Anderson Msumba katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, wamehimizwa kuendelea kutoa ushirikiano katika suala la chakula shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha kutosha wakati wa masomo.

Ushirikiano huo unalenga kuwawezesha wanafunzi kuwa na afya njema na utayari wa kujifunza, hivyo kuongeza bidii katika masomo na hatimaye kuboresha ufaulu wao kitaaluma.

Wito huo umetolewa leo na mgeni rasmi ambaye ni pia diwani wa kata ya Nyihogo Sindano William, wakati wa mahafali ya 2 ya shule hiyo, ambapo amesema wazazi wanapaswa kuona suala la chakula shuleni ni sehemu muhimu ya malezi na kwa kushirikiana na uongozi wa shule katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.

Sauti ya diwani wa kata ya Nyihongo Sindano William

Aidha, Sindano ameutaka uongozi wa Serikali wa Mtaa wa Nyihogo kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo kuandaa Kikao cha pamoja kitakachokuja na Suluhu ya Changamoto zinazoikabili Shule ya Sekondari Anderson Msumba zilizowasilishwa katika risala.

Sauti ya diwani wa kata ya Nyihongo Sindano William

Naye, Makamu Mkuu wa Shule ya sekondari Anderson Msumba Mohammed Masunga wameeleza namna shule inavyopiga hatua mbalimbali, huku akitaja Changamoto zinazoikabili Shule hiyo ikiwemo ukosefu wa Jengo la Utawala, upungufu wa majengo ya Maabara,na Maktaba.

Sauti ya Makamu Mkuu wa Shule ya sekondari Anderson Msumba Mohammed Masunga

Awali, katika risala ya wahitimu iliyosomwa na Halima Maganga amesema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali mojawapo ni kwa baadhi ya wanafunzi pindi masomo yanapoendelea kutokupata chakula shuleni pamoja na upungufu wa walimu na kuomba changamoto kutatuliwa ili kuongeza ufaulu shuleni hapo.

Sauti ya msoma risala Halima Maganga

Katika Mahafali ya Pili ya Kidato cha Nne Shule ya Sekondari Anderson Msumba Mwaka 2026 Jumla ya Wanafunzi 295 wamehitimu masomo na kutunukiwa Vyeti na Zawadi mbalimbali kutoka kwa Uongozi wa Shule hiyo.