Kahama FM
Kahama FM
27 October 2026, 5:03 pm

“Tunatoa elimu hii, ili msije kujiingiza kwenye mambo mabaya na kuharibikiwa mkiwa hapa chuoni, tabia ambazo hamkutoka nazo nyumbani kwenu”
Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM) wamepewa elimu ya kukabiliana na vitendo vya ulevi, mapenzi ya jinsia moja, uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuepuka kutumia vibaya mitandao ya kijamii.
Elimu hiyo imetolewa na maafisa wa Jeshi la Polisi, waliofika chuoni hapo kutoa elimu hiyo kupitia kampeni ya kuzungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza, wanaoripoti vyuoni kuanza masomo, kwa lengo la kuwasaidia kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wao na kuathiri masomo yao.

Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Shinyanga Fraterine Tesha, amesema wametoa elimu kwa wanafunzi hao, ili kuwajengea uelewa wa kuepuka kujiingiza katika vitendo hivyo, ambavyo wanaweza kuviinga na kujikuta wakipoteza ndoto zao.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Shinyanga (OCD) Stephen Kimaro, amewataka wanafunzi hao kujiepusha na vitendo vya uhalifu, ikiwamo kutoibia kompyuta mpakato (laptop), ubakaji, ulawiti na kutosambaza picha chafu kwenye mitandao ya kijamii.
Baadhi ya wanafunzi hao, akiwamo Salama Salumu, wamesema elimu waliyopewa na Jeshi la Polisi, imewasaidia kuelewa namna ya kujilinda na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wao wanapokuwa chuoni na wanapoendelea na masomo yao.
