Kahama FM
Kahama FM
11 November 2026, 11:40 pm

‘‘Uchimbaji madini kuwa shughuli inayoweza kuleta kipato, haipaswi kuwa kikwazo kwa watoto kupata elimu, kwani elimu ndiyo msingi wa maisha na inaweza kuwasaidia kujitegemea hata baada ya shughuli za uchimbaji kusimama’’
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka wazazi na walezi katika maeneo yanayojishughulisha na uchimbaji madini kuhakikisha watoto wanaendelea na masomo badala ya kuvutiwa na shughuli za uchimbaji madini na kuacha shule.
Dkt. Nchemba ametoa wito huo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Segese, Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, katika mkutano wa hadhara, akieleza kuwa madini ni rasilimali zinazoweza kuisha, hivyo elimu ni msingi muhimu wa kuwaandaa watoto kukabiliana na maisha hata baada ya shughuli za uchimbaji kusimama.

Amesisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuwahimiza watoto kusoma na kutumia muda wao vizuri, kwani elimu inaweza kuwafungulia fursa mbalimbali za kiuchumi hata baada ya rasilimali za madini kumalizika.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mabula Magangila, ameiomba Serikali kuwezesha kuanzishwa kwa kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika eneo la Msalala ili kutoa mafunzo ya taaluma ya madini na kuwawezesha vijana kupata elimu ya nadharia na vitendo bila kuacha masomo.
Mabula amesema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikataa kwenda shule na kuvutiwa na shughuli za uchimbaji mdogo wa madini wakiamini masomo yanawachelewesha kupata kipato.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Segese, akiwemo Nairo Kampunduji na Faida William, wameunga mkono msisitizo huo wa Waziri Mkuu, wakieleza kuwa elimu ndiyo msingi wa maisha na ni jukumu la wazazi kuhakikisha watoto wanapata fursa ya kusoma.
Wananchi hao wamewataka wazazi na walezi kuendelea kuipa elimu kipaumbele na kutoruhusu shughuli za kiuchumi, hususan uchimbaji madini, kuwa sababu ya watoto kukatisha masomo yao.