Kahama FM
Kahama FM
9 November 2026, 1:04 am

‘‘Hatua hiyo inalenga kutatua malalamiko ya wakulima kuhusu mfumo wa mnunuzi mmoja’’
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaruhusu wanunuzi mbalimbali kushiriki katika ununuzi wa pamba kuanzia msimu ujao, hatua inayolenga kuongeza ushindani wa bei na kuwawezesha wakulima kunufaika zaidi na mazao yao.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya SHIRECU, wilayani Kishapu, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Shinyanga.

Dkt. Mwigulu amesema kuanzia msimu ujao hakutakuwa na mfumo wa mnunuzi mmoja, bali wanunuzi mbalimbali wataruhusiwa kununua pamba ili kuongeza ushindani na kuchochea kupanda kwa bei ya zao hilo.
Amesema hatua hiyo inalenga kutatua malalamiko ya wakulima kuhusu mfumo wa mnunuzi mmoja, ambayo pia yaliwasilishwa na Mbunge wa Kishapu, Lucy Thomas Mayenga.

Awali, Mayenga amesema mfumo huo umekuwa ukiwanyima wakulima uhuru wa kuchagua wanunuzi na kujadiliana bei, huku baadhi yao wakikumbana na changamoto wanapojaribu kutafuta masoko ya pamba katika maeneo mengine.