Kahama FM
Kahama FM
15 October 2026, 11:28 am

‘‘Akihimiza wananchi kutambua madhara ya ukiukwaji wa sheria na kuepuka kuhalalisha vitendo hivyo’’
Naibu Kamishna wa Polisi, DCP Henry Mwaibambe, amewaonya vijana nchini kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi, badala yake wawe daraja la kuwasaidia kutimiza ndoto zao za kielimu.
Mwaibambe, ambaye pia ni Mkuu wa Ushirikishwaji wa Polisi Jamii kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, ametoa onyo hilo leo, wakati akizungumza na madereva wa bodaboda katika kijiji cha Kakola, kata ya Bulyanhulu, Halmashauri ya Msalala.

Aidha, amesema watoto wa shule wanahitaji kulindwa ili waweze kutimiza malengo yao ya kielimu na kujenga maisha bora ya baadaye, huku akisisitiza kuwa jamii inapaswa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kupambana na vitendo vinavyohatarisha usalama na mustakabali wa watoto.
Kwa upande wake, mmoja wa madereva wa bodaboda, Nuru Ramadhani, mkazi wa Kakola, ameeleza kufurahishwa na ziara hiyo, akisema falsafa ya Polisi Jamii imechangia kuimarisha uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi kuimarisha ushirikiano na wananchi katika kuzuia uhalifu na kujenga jamii salama kupitia falsafa ya Polisi Jamii.