Kahama FM
Kahama FM
19 September 2026, 11:04 pm

‘‘Mfuko umewataka wanachama na wananchi kwa ujumla kuwa makini na watu wanaodai kutoa huduma za PSSSF nje ya njia rasmi, na kuhakikisha wanathibitisha huduma wanazohitaji kupitia ofisi au njia rasmi za mfuko’
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetoa tahadhari kwa wananchi, hususan wastaafu na wanachama wake, dhidi ya watu wanaodai kuwa mawakala wa mfuko huo na kutoa huduma kwa niaba ya PSSSF.
Akizungumza katika semina waandishi wa habari wa mkoa wa Shinyanga na Simiyu, Afisa Msimamizi wa PSSSF Mkoa wa Simiyu, Salum MWEGELO amesema mfuko huo hauna mawakala wanaotoa huduma kwa niaba yake popote nchini.

Amesema huduma za PSSSF zinapatikana kupitia ofisi rasmi za mfuko zilizopo katika mikoa mbalimbali nchini, huku akisisitiza umuhimu wa wanachama kutumia njia rasmi za kupata huduma za mfuko huo ili kujilinda dhidi ya utapeli, wizi wa fedha na matumizi mabaya ya taarifa zao binafsi.
Aidha, Mwegelo amewahimiza wanachama kutumia mifumo ya kidijitali kuhakiki taarifa za michango na mafao yao mapema ili kubaini makosa na kuepuka changamoto wakati wa kudai mafao.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mfawidhi PSSSF Shinyanga, Sunday Rashid, amesema mfuko umeanza kushughulikia taarifa za watumishi wanaokaribia kustaafu miezi sita kabla ya tarehe yao rasmi ya kustaafu ili kutoa muda wa kuhakiki taarifa na kurekebisha changamoto.

Naye Mratibu wa TBN Kanda ya Ziwa, Kadama Malunde, amewasisitiza waandishi wa habari kutumia taaluma yao kuwafikishia wananchi elimu sahihi kuhusu haki, wajibu na huduma za hifadhi ya jamii.