Kahama FM
Kahama FM
16 September 2026, 2:32 pm

‘‘Wananchi endelea kushiriki katika kukamilisha ujenzi huo, ambao unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza usalama kwa wanafunzi’’
Wananchi wa Kata ya Nyandekwa pamoja na wadau mbalimbali katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, wamechangia zaidi ya shilingi milioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Nyandekwa.
Fedha hizo zimetolewa kupitia harambee iliyoandaliwa na Diwani wa Kata ya Nyandekwa, ikiwa na lengo la kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi, hususan wanafunzi wa kike, ambao hulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni.

Akizungumza katika harambee hiyo, mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, aliyewakilishwa na Afisa Elimu ya Watu Wazima wa Mkoa wa Shinyanga, Didani Lutazika, amewataka wananchi na wadau kuhakikisha fedha zilizopatikana zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, Lutazika amesisitiza kuundwa kwa kamati ya ujenzi itakayohusisha wadau na wananchi, huku akitaka kuwepo kwa uwazi na utoaji wa taarifa kuhusu matumizi ya fedha pamoja na maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo.

Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Nyandekwa Rutahondi Katoto amesema kuwa jengo hilo lilikuwepo kipindi anasoma katika shule hiyo na kuwaomba wananchi na wadau wa maendeleo kuchangia ujenzi wa boma hilo likamilike ili serikali kulimalizia hatua inayofuata na lianze kutumia.

Naye, Diwani wa kata ya Igunda halmashauri ya Ushetu Tabu Katato, wakati akichangia ujenzi wa majengo hayo amesema kuwa wananchi wanapaswa kushirikiana katika suala la maendeleo pasipo kuangalia eneo unalotokea.

Awali, Mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyandekwa Happynes Dalali akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wezake, amesema shule hiyo imekuwa kiendelea kupata ufauli mzuri, huku akikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikwemo ya ukosefu wa mabweni ya wanafunzi pamoja na jengo la utawala.
Wananchi na wadau mbalimbali wameendelea kuhamasishwa kushiriki katika kukamilisha ujenzi huo, ambao unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza usalama wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyandekwa, huku ujenzi huo unakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 50.
