Kahama FM

Wazazi Ushetu, watakiwa kuwekeza elimu kwa watoto wao

5 September 2026, 1:03 am

Mkuu wa shule ya sekondari ya Ushetu Helen Dotto Stima akizungumza na wanafunzi na wazazi katika mahafali ya kidato cha nne katika shule hiyo (Picha na Sebastian Mnakaya)

‘‘Wazazi somesheni watoto wenu ili watimize ndoto zao’’

Wazazi na walezi katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuacha tabia ya kuwaozesha watoto wao kwa lengo la kutafuta mali, na badala kuwapa nafasi ya kusoma ili waweze kutimiza ndoto zao.

Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa shule ya sekondari ya Ushetu Helen Dotto Stima, wakati wa mahafali ya 15 wa shule hiyo, ambapo amesema kuwa wazazi wanapaswa kuwapa fursa watoto wao kupata elimu na kuachana na mila na desturi zitakazomzuia motto kupata elimu.

Aidha, jamii imetakiwa kushirikiana katika kuhakikisha watoto wao wanalindwa na kuachana na kuwaoza, na badala yake wanawapatia mazingira salama ya kusoma na kufikia malengo yao.

Sauti ya Mkuu wa shule ya sekondari ya Ushetu Helen Dotto Stima

Mgeni rasmi katika mahafali hayo mbunge wa jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani, akiwakilishwa na katibu wa Jimbo hilo Richard Gwesa, amesema kuwa dunia sasa inahitaji wasomi na kuwataka wazazi na walezi suala ya elimu liwe kipaumbele kwa watoto, huku serikali ikiendelea kuboresha kila siku kwenye sekta elimu.

Sauti ya katibu wa mbunge wa Jimbo la Ushetu Richard Gwesa

Akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzake wa kidato cha nne Rhoda Masanja, amesema kuwa shule hiyo ina changamoto mbalimbali, ikiwemo kutokuwa na upatikanaji wa maji safi, ukosefu wa walimu kwa baadhi ya masomo na baadhi ya wanafunzi kuacha masomo kwa sababu mbalimbali.

Sauti ya msoma risala Rhoda Masanja

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Ushetu wakizungumza kwa nyakati tofauti, wamewaomba wazazi wao kuwapa nafasi zaidi katika kipindi cha kusubiri matokeo wa mitihani yao ili waendele na masomo ya kidato cha tano ama kwenda chuo na wasiwaozeshe.

Sauti za wanafunzi wa shule ya sekondari Ushetu

Ikumbukwe, shule ya sekondari Ushetu ilianzishwa mwaka 2009, leo ikiwa na mahafali ya 15, ambapo ikiwa na jumla ya wanafunzi 40 wa kiume 20 na wakie 20 wanotarajiwa kuhitimu mwaka huu 2026.