Kahama FM

Diwani akabidhi uwanja wa michezo kwa vijana

24 September 2026, 4:11 pm

Diwani wa Kata ya Nyihogo Sindano William na vijana wa kata hiyo baada ya kuwakabidhi uwanja huo ambao wataanza kufanya mazoezi baada ya kukamilika kufanyiwa usafi (Picha na Sebastian Mnakaya)

‘‘Eneo hilo lipo karibu na Bwawa la Nyihogo, hali iliyosababisha vijana kukosa sehemu rasmi ya kufanyia mazoezi na kuendesha shughuli za michezo’’

Vijana wa Kata ya Nyihogo, katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wamekabidhiwa uwanja wa mpira kwa ajili ya mazoezi na kuendeleza vipaji vya michezo, huku wakichangiwa zaidi ya shilingi milioni moja kwa ajili ya kuushafisha uwanja huo.

Uwanja huo umekabidhiwa na Diwani wa Kata ya Nyihogo Sindano William, kupitia ruhusa iliyotolewa na Bonde la Maji la Ziwa Tanganyika, baada ya eneo hilo kwa zaidi ya miaka minne kutotumika kwa shughuli za michezo, ingawa awali lilikuwa likitumika na timu ya mpira ya Nyihogo United.

Diwani wa Kata ya Nyihogo Sindano William akikagua uwanja huo baada ya kuwakabidhi vijana hao

Awali, eneo hilo lilikuwa limetengwa kwa ajili ya shughuli za uhifadhi wa vyanzo vya maji, ikiwemo upandaji wa miti, huku shughuli za kibinadamu zikizuiwa kutokana na kuwa karibu na Bwawa la Nyihogo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Diwani wa Kata ya Nyihogo Sindano amesema kurejeshwa kwa uwanja huo kutawasaidia vijana kupata eneo la kufanya mazoezi na kutumia muda wao katika shughuli za michezo.

Sauti ya Diwani wa Kata ya Nyihogo Sindano William

Aidha, Diwani Sindano amesema hatua hiyo pia inalenga kuwasaidia vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na mihadarati, pamoja na vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi kwa kuruhusiwa kuutumia uwanja huo.

Sauti ya Diwani wa Kata ya Nyihogo Sindano William

Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa timu ya Nyihogo united wakizungumza baada ya kukabidhiwa uwanja huo, wamesema memshukuru diwani huyo kwa kuwapambania kufanikisha kukabdihiwa kuanza kuutumia hali itakayowasaidia kutojiingiza katika makundi yasiofaa.

Sauti za viongozi mbalimbali wa timu ya Nyihogo United

Nao, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Nyihogo akiwemo katibu Thomas Shaban na wenyekiti wa tawi la Sazia Adam Hamis wameishukuru serikali kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akiwaomba vijana kuendelea kuwa wavumilivu wakati wa kushughulia changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Sauti za viongozi mbalimbali wa CCM kata ya Nyihogo

Uwanja huo uliwahi kutumiwa na vijana wa eneo hilo kwa ajili ya mazoezi kabla ya kusitishwa kwa matumizi yake kutokana na masharti ya uhifadhi wa eneo hilo.