Kahama FM
Kahama FM
12 November 2026, 1:19 am

Tanroads yaagizwa kuharakisha usanifu wa barabara ya Kahama–nyamilangano, Ushetu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuharakisha usanifu wa kina wa barabara inayounganisha Halmashauri ya Ushetu na Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, ili iweze kuingizwa katika mipango ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha.
Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Nyamilangano, Halmashauri ya Ushetu, ambapo amemtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga kuongeza kasi ya kazi hiyo kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha usanifu unakamilika kwa wakati.

Akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa agizo hilo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesye, amesema usanifu wa kina wa barabara hiyo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi minne.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, alimuomba Waziri Mkuu kuhakikisha barabara inayotoka Kahama Mjini kuelekea Nyamilangano, Ushetu, inajengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri na usafirishaji pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.