Kahama FM
Kahama FM
7 October 2026, 1:48 pm

Jeshi la Polisi Wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga, limewataka watumiaji wa vyombo vya moto, ikiwemo pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda, kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani ili kujilinda wao pamoja na watumiaji wengine wa barabara.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Polisi Manispaa ya Kahama, SSP Maro Kenyunko, wakati akizungumza na baadhi ya waendesha pikipiki za abiria waliokamatwa kwa makosa mbalimbali, ikiwemo kutovaa kofia ngumu na kutoweka namba za usajili kwenye vyombo vyao.

Kwa upande wake,Mkuu wa Usalama Barabarani Manispaa ya Kahama, Flora Nangale, amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua dhidi ya madereva na watumiaji wengine wa vyombo vya moto wanaokiuka sheria za usalama barabarani.

Baadhi ya madereva wa pikipiki za abiria wamewaasa wenzao kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, wakieleza kuwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza makosa na kuimarisha usalama barabarani.
Jeshi la Polisi Wilaya ya Kahama limeeleza kuwa zoezi hilo ni endelevu, huku likisisitiza kuwa vyombo vyote vya moto, vya umma na binafsi, vitakavyobainika kufanya makosa vitachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
