Kahama FM
Kahama FM
24 October 2026, 2:09 am

‘‘Mpango Kabambe kuzingatia mahitaji ya huduma za kijamii kwa miaka 25 ijayo, yakiwemo maeneo ya shule za sekondari na shule za msingi, pamoja na maeneo ya makaburi ya umma, kutokana na ongezeko la wakazi na uhaba wa maeneo’’
Wananchi wa Kata ya Mhungula, katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wamependekeza maeneo ya ujenzi wa kituo cha polisi, zahanati pamoja na shule za msingi na sekondari kuingizwa katika Mpango Kabambe wa matumizi bora ya ardhi ili kukidhi mahitaji ya huduma za kijamii kwa miaka 25 ijayo.
Wakizungumza katika kikao cha Kupanga Kahama ya Baadaye, wananchi hao wamesema ongezeko la wakazi na matukio ya kiuhalifu katika maeneo mbalimbali yanaongeza umuhimu wa kuwa na kituo cha polisi kilicho karibu na wananchi, hivyo wameiomba Serikali kuzingatia pendekezo hilo katika ramani ya Mpango Kabambe wa kidijitali kabla ya kuanza kwa utekelezaji wake.

Aidha, wananchi hao wameeleza umuhimu wa Mpango Kabambe kuainisha maeneo ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari, zahanati pamoja na makaburi ya umma, wakisema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na uhaba wa maeneo ya huduma za kijamii unaochangiwa na ongezeko la wakazi.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Prosper Mlacha, amesema Mpango Kabambe ni mpango shirikishi unaozingatia maoni, mahitaji na maono ya wananchi, hivyo mapendekezo yaliyotolewa katika kikao hicho yatapitiwa na kufanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha matumizi ya ardhi na kuongoza maendeleo ya mji wa Kahama.
Amesisitiza kuwa upangaji mzuri wa matumizi ya ardhi utasaidia kuhakikisha kuwa Manispaa ya Kahama inakuwa na maendeleo yaliyopangwa vizuri na miundombinu inayokidhi mahitaji ya wananchi kwa sasa na katika kipindi cha miaka 25 ijayo.
