Kahama FM
Kahama FM
21 November 2026, 4:40 pm

‘‘Makampuni ya ulinzi yanapaswa kuepuka kuajiri wafanyakazi kiholela na kuhakikisha zinafuata taratibu zilizowekwa ili kuzuia hali ya walinzi wenyewe kuhusika katika vitendo vya wizi wanapokuwa kazini’’
Jeshi la Polisi Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga limezitaka kampuni za ulinzi zinazofanya shughuli zake katika eneo hilo kuzingatia taratibu na masharti yaliyowekwa katika vibali vyao, ikiwemo uhakiki wa taarifa za watu kabla ya kuwaajiri pamoja na matumizi sahihi ya silaha.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Manispaa ya Kahama, OCD SSP Maro Kenyuko, wakati wa hafla ya kusherekea miaka 10 ya kuanzishwa kwa kampuni ya ulinzi ya Dyanabo Fabian, ambapo amezisisitiza kampuni za ulinzi zinapaswa kufanya uchunguzi wa kina kwa watu wanaowaajiri ili kuhakikisha wanakuwa na uadilifu na sifa zinazostahili kabla ya kuwapangia majukumu ya ulinzi.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuzuia vitendo vya wizi vinavyoweza kufanywa na baadhi ya walinzi wanaoajiriwa bila kufanyiwa uhakiki wa kutosha.
Aidha, amezitaka kampuni hizo kuacha tabia ya kuazimana silaha za moto bila kufuata utaratibu wa Jeshi la Polisi, akieleza kuwa silaha hutolewa kwa matumizi maalumu na kwa mtu aliyeidhinishwa, hivyo matumizi yake kinyume na masharti ni kosa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni za ulinzi ya Dyanabo Fabian iliyoopo Kahama, amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa maelekezo hayo, akisema yana umuhimu katika kuhakikisha kampuni za ulinzi zinafuata masharti ya vibali vyao na kudhibiti vitendo vya uhalifu.
Hata hivyo, ameziomba kampuni nyingine za ulinzi kuzingatia maelekezo hayo kwa kuhakikisha zinakuwa na mifumo mizuri ya usimamizi wa wafanyakazi na matumizi ya silaha kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
