Kahama FM

Wananchi Jana Wapongeza Ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Buluma ya Sh Milioni 130

29 September 2026, 11:28 am

Diwani wa Kata ya Jana, Shigela Sonda akizungumza na wananchi wa kata hiyo wakati wakikagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari Buluma (Picha na Sebastian Mnakaya)

‘‘shule mpya ya sekondari buluma kupunguza umbali wa wanafunzi kutembea zaidi ya km 18’’

Wananchi wa Kata ya Jana katika halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameeleza kuwa ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika eneo la Buluma utasaidia kupunguza changamoto ya umbali kwa wanafunzi wanaotembea zaidi ya Km 18 kwenda shule kutokea maeneo ya mbalimbali ya kata hiyo wenye thamani ya shilingi 130.

Akizungumza wakati wa kuanzishwa kwa mradi huo, Diwani wa Kata ya Jana, Shigela Sonda, amesema kata hiyo ni kubwa na baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutoka maeneo ya Izuga na Matinje kwenda shule ya sekondari ya Jana.

Aidha, Shigela amesema uamuzi wa kujenga sekondari ya pili umetokana na mahitaji ya wananchi, ambao walihitaji huduma ya elimu kusogezwa karibu na makazi yao, huku akiwashukuru viongozi wa serikali, akiwemo Mbunge wa eneo hilo, kwa kushirikiana na wananchi katika kufanikisha mradi huo.

Sauti ya Diwani wa Kata ya Jana, Shigela Sonda

Kwa upande wake, mkuu wa shule ya sekondari Jana Felista Barnaba, amesema kuwa ujenzi huo ukikamilika utaweza kuwasidia wanafunzi kutokutembea mbali, huku akiwataka wazazi kuwasimamia watoto wao kusoma ili watimize ndoto zao.

Sauti ya mkuu wa shule ya sekondari Jana Felista Barnaba

Nao, baadhi ya wazazi katika kata hiyo wakizungumza kwa nyakati tofauti akiwemo Abudila Bundala, Hellena Dotto na Peter Nangu ameishukuru serikali kwa kuanza kwa ujenzi huo wa shule ya sekondari ambayo itawasaidia watoto kutokutembea umbali mrefu, huku wakisema kuwa wako tayari kuchangia ujenzi huo.

Sauti ya wazazi kwa kata ya jana, akiwemo Abudila Bundala, Hellena Dotto na Peter Nangu

Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuuwezesha mradi huo kufika katika Kata ya Jana, huku akiwataka wananchi kushirikiana katika kuhakikisha ujenzi na maendeleo ya shule hiyo yanafanikiwa.