Kahama FM
Kahama FM
25 November 2026, 2:39 pm

Kahama kununua mitambo ya kutengeneza barabara za mitaa
Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imepata kibali cha kununua mitambo ya kutengeneza barabara, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya ubovu wa barabara za mitaa na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masud Kibetu, ameyasema hayo wakati akijibu swali la Diwani wa Kata ya Majengo, Zacharia Soko, katika kikao cha Baraza la Madiwani, aliyetaka kujua ni lini Halmashauri itakamilisha ununuzi wa mitambo hiyo.

Kibetu amesema kuchelewa kwa ununuzi wa mitambo hiyo kulitokana na changamoto ya kutopatikana kwa kibali, lakini kwa sasa kibali hicho kimepatikana na utekelezaji wa zoezi la ununuzi unatarajiwa kuanza ndani ya wiki mbili.
Awali, Diwani wa Kata ya Majengo, Zacharia Soko, aliitaka Halmashauri kutoa ufafanuzi kuhusu lini mitambo hiyo itanunuliwa, akieleza umuhimu wake katika kukabiliana na changamoto ya ubovu wa barabara za mitaa katika Manispaa hiyo.

Halmashauri ya Manispaa ya Kahama katika mwaka wa fedha 2026/2027 imetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitambo hiyo, huku hatua za utekelezaji zikiendelea ili kuhakikisha inapatikana kwa wakati na kusaidia kuboresha miundombinu ya barabara.