Kahama FM
Kahama FM
18 October 2026, 12:23 am

Miradi ya maendeleo kahama yafikia asilimia 61 ya utekelezaji
Na Sebastian Mnakaya
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Florent Kyombo, amewataka viongozi wa mkoa wa Shinyanga kusimamia kwa karibu miradi ya maendeleo ya kimkakati inakamilika kwa wakati na kwa mujibu wa mikataba iliyosainiwa na wakandarasi.
Kyombo ametoa wito huo wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya Bunge ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Manispaa ya Kahama, ambapo amesema kwa wastani miradi hiyo imefikia asilimia 61 ya utekelezaji.

Amesema ni muhimu kwa viongozi kuendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo, huku akiwapongeza wakandarasi na washauri elekezi kwa juhudi wanazozifanya, pamoja na serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo.
Aidha, ameeleza kuwa lengo ni kuhakikisha miradi inakamilika ndani ya muda wa mikataba ili wananchi waweze kupata huduma zilizokusudiwa na kunufaika na maendeleo yanayotekelezwa katika maeneo yao.

Kwa upande wake Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Pili Mnyema amasema Serikali ya mkoa huo imepokea maelekezo ya kamati, huku ikiahidi kusimamia miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kuanza kuwahudumia Wananchi.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI Hawa Subira Mwaifunga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, ameupongeza uongozi wa Manispaa ya Kahama kwa kusimamia vizuri miradi ya maendeleo, huku meya wa Manispaa hiyo Mataluma Kaniki amesema ni muhimu kuhakikisha wafanyabiashara wanapata vibanda katika stendi hiyo kwa utaratibu wa haki, uwazi na bila upendeleo
Jumla ya Miradi minne yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 27 ikiwemo jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Stendi na Soko yaliyopo katika eneo la Dodoma Viwandani-Zongomela, Soko la Sango-Nyasubi na Stendi kuu ya Mabasi iliyopo Mbulu.
