Kahama FM
Kahama FM
2 November 2026, 1:16 pm

Kahama 2050, wananchi wataka barabara, mifereji na vituo vya afya
Wananchi na viongozi wa Kata wa Majengo katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, wameiomba Serikali kuhakikisha Mpango Kabambe wa Mji wa Kahama kuelekea mwaka 2050 unazingatia ujenzi wa barabara zenye mifereji ya maji, njia za watembea kwa miguu pamoja na upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii, ikiwemo vituo vya afya.
Wamesema uwepo wa miundombinu hiyo utasaidia kupunguza mafuriko yanayosababishwa na kuzibwa kwa njia za maji, ajali za barabarani pamoja na changamoto za utoaji wa huduma za dharura, hususan wakati wa majanga ya moto.

Akizungumza kuhusu changamoto za mifereji ya maji, katika kikao cha kupanga Kahama ya baadae, baadhi ya wananchi akiwemo Hamis Masudi Chanda na Laurent Nkwabi wamesema baadhi ya maeneo yamejengwa bila kuzingatia njia za asili za maji, hali inayosababisha maji kuelekezwa kwenye makazi ya wananchi.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Majengo, William Mzava, amesema ongezeko la watu na ujenzi usiopangwa vimeongeza changamoto za matumizi ya ardhi, ikiwemo ubana wa barabara, ukosefu wa nafasi za kutosha za huduma za kijamii na ugumu wa vyombo vya uokoaji kupita wakati wa dharura.
Nae, Mtaalumu wa Maendeleo ya Jamii na Usalama kutoka Urban Solution, Novatus Kaijage amesema kuwa kabla ya watu kuongezeka kwa kasi katika mji wa Kahama inapaswa kupangwa mapema ili kuondokana na migogoro aridhi itakayojitokeza hapo baadae.

Mpango Kabambe wa Mji wa Kahama wa mwaka 2025 hadi 2050 unalenga kuweka utaratibu wa matumizi bora ya ardhi na kuongoza maendeleo ya mji kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wananchi.