Kahama FM

Katibu wa Baraza la Wazee Taifa atoa ajenda tano za kuboresha maisha ya wazee

11 October 2026, 4:08 am

Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, Andarson Lymo (Picha na Sebastian Mnakaya)

Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, Andarson Lymo, ameeleza ajenda tano zinazolenga kuboresha maisha ya wazee nchini, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa sheria maalumu ya wazee, malipo ya pensheni, huduma bora za afya, ushirikishwaji wa wazee katika maamuzi na uhakika wa usalama wa kipato.

Lymo ameeleza ajenda hizo wakati akizungumza na kituo cha redio cha Kahama FM, akibainisha kuwa utekelezaji wake unalenga kupunguza na kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee, ikiwemo zile zinazohusishwa na kutokuwepo kwa sheria maalumu inayolinda na kusimamia haki zao.

Amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sheria ya wazee itakayoweka utaratibu wa kulinda haki zao, pamoja na kuhakikisha wanapata huduma za afya zilizo bora, kipato cha uhakika na nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu maisha yao na jamii kwa ujumla.

Nae, mzee Jumanne Kasuku anayeishi katika kata ya Nyahanga Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga aliyestaafu miaka 12 iliyopita katika idara ya mifugo ameeleza namna sheria hiyo ikiwepo itaweza kuwasaidia wazee kwa kiasi kikubwa katika kutatua changamoto zao mbalimbali zinazowakabili kwa sasa.

Sikiliza kipindi cha Meza ya Jamii kinacholetwa kwenu na Sebastian Mnakaya kizungumza na wazee