Kahama FM
Kahama FM
10 November 2026, 11:38 pm

Sekta ya afya nchini imeendelea kufanya mageuzi makubwa kupitia uboreshaji wa miundombinu na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa, hatua inayolenga kuongeza ubora wa huduma za matibabu kwa wananchi
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kwa kutumia mapato ya ndani kuboresha miundombinu ya sekta ya afya, hatua inayolenga kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.
Dkt. Nchemba ametoa pongezi hizo wakati akikagua ujenzi wa jengo jipya la Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ambapo amesema ameridhishwa na uwekezaji unaofanyika kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatambua na kuthamini mchango wa watumishi wa afya katika kuboresha huduma kwa wananchi, huku akisisitiza kuwa sekta hiyo ni miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele na Serikali.
Aidha, Dkt Nchemba amesema Serikali itaendelea kuboresha maeneo ambayo bado yanachangamoto ili kuhakikisha watumishi wa afya wanatoa huduma katika mazingira bora na yenye vifaa vinavyokidhi mahitaji ya wananchi.

Awali, mganga mkuu wa hospitali ya Manispaa ya Kahama Dkt Baraka Msumi amesema wanathamini jitihada zilizofanyika katika kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza uwezo wa vituo vya kutolea huduma za afya katika Manispaa ya Kahama.

Mhandisi wa Manispaa ya Kahama Mashala Mboje, akisoma taarifa ya mradi huo amesema kuwa jengo jipya la huduma za mama na mtoto linajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 6.79, huku Serikali Kuu ikichangia shilingi bilioni moja na mapato ya ndani ya Manispaa ya Kahama yakichangia sehemu iliyobaki.
Mradi huo ulioanza Januari 23, 2023, umefikia asilimia 70 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Juni 4, 2027.